Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Juni 09, 2023 Local time: 10:08

Wanigeria waandamana kupinga ongezeko la bei ya mafuta


Waandamanaji wakishikilia mabango kupinga ongezeko la bei ya mafuta katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos, Nigeria

Watu kadhaa wamekufa nchini Nigeria kufuatia mapambano kati ya polisi na wananchi

Maelfu ya wa-Nigeria wanapinga kupanda kwa bei ya mafuta, na kuzusha mapambano na polisi ambayo yameuwa watu wasiopungua watatu.

Mashahidi wanasema afisa mmoja wa polisi alimfyatulia risasi na kumuuwa mwandamaji mmoja Jumatatu katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos.

Kwingineko mjini humo, polisi wa kutuliza ghasia walisimama kuangalia wakati waandamanaji walipofunga barabara, kuchoma matairi na kuimba wimbo dhidi ya sera za Rais Goodluck Jonathan.

Huko kaskazini katika mji wa Kano, mashahidi wanasema watu wawili waliuwawa wakati wa maandamano. Shirika la Msalaba Mwekundu linaripoti kuwa watu wasiopungua 14 walijeruhiwa, wakiwemo saba ambao wameathiriwa na majeraha ya risasi.

Maafisa wa jimbo la Kano wameweka marufuku ya kutotoka nje kwa saa 14, kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa mbili asubuhi kwa saa za Nigeria, katika juhudi za kurejesha amani.

Maelfu ya wa-Nigeria walianza mgomo wa kitaifa Jumatatu, wakipinga uamuzi wa serikali wa wiki iliyopita wa kusitisha ruzuku ya mafuta. Bei ya mafuta imepanda mara mbili katika siku moja kwa takriban senti 88 kwa lita moja.

Maandamano yalisimamisha shughuli katika baadhi ya miji, ikiwemo mji mkuu Abuja. Vyama vikuu vya wafanyabiashara nchini humo viliitisha mgomo ili kuishinikiza serikali kurudisha ruzuku.

Msemaji wa chama cha National Labor Congress, Owen Lakemfa, aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kuwa serikali imekataa juhudi za vyama hivyo za kuanza tena mazungumzo juu ya suala hilo.

Serikali inaahidi kutumia dola bilioni 8 ilizoziokoa ili kuwekeza katika program za miundo mbinu na kijamii nchini humo.

Ruzuku ya mafuta ilikuwa moja ya maslahi machache ambayo wa-Nigeria wanayapata kutoka kwenye nchi yao yenye utajiri wa mafuta. Watu wengi nchini Nigeria wanaishi chini ya zaidi ya dola mbili kwa siku.

XS
SM
MD
LG