Rais wa Niger Mahamadou Issoufou alisema Ujerumani inaweza kujenga kituo cha kijeshi nchini humo wakati ikiwa katika harakati za kuongeza nguvu za mapambano dhidi ya wenye itikadi kali katika taifa hilo la Afrika magharibi na pia jirani na nchi ya Mali.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press-AP, Rais Issoufou alizungumza hayo akiwa na Chansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambaye yupo nchini humo kama sehemu ya ziara yake ya mataifa matatu ya Afrika magharibi.
Bwana Issoufou alisema changamoto mpya zinatupa mbinu za kupanua ushirikiano wetu wa pamoja, kuelezea masuala ya nchi yanayohusu usalama na wahamiaji wakati ambapo tunashirikiana mipaka na nchi ya Libya na Chad.
Aliongeza kusema kwamba tutaipatia Ujerumani eneo kwa ajili ya kituo cha mikakati ya kusaidia kupeleka vifaa kwa wanajeshi wake nchini Mali ili kupambana dhidi ya ugaidi.
Ujerumani ina kiasi cha wanajeshi 650 wanaounga mkono operesheni za walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali.