Sehemu ya matokeo ya Uchaguzi wa urais wa Nicaragua inaonyesha Daniel Ortega akielekea kushinda kwa muhula wa tatu. Huku asilimia 21ya kura zikiwa zimehesabiwa, mkuu wa baraza la uchaguzi Roberto Rivas amesema Jumapili kuwa Rais Ortega tayari amepata zaidi ya asilimia 71ya kura zilizopigwa.
Rivas ameambia wanahabari kuwa asilimia 65 ya wapiga kura milioni 3.8 walioandikishwa wameshiriki uchaguzi huo akiongeza kuwa matokeo yanatarajiwa baadaye leo. Kulingana na ripoti zilizotolewa,Ortega ambae alikuwa mwanajeshi wa uwasi wakati mmoja anatarajiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura kwenye uchaguzi huo ulio na wagombea watano wa urais.
Naibu Rais wa Ortega ni mke wake Rosario Murillo. Baada ya kupiga kura Jumapili, Ortega na mkewe Murillo walisema kuwa uchaguzi huo utaweka historia isiyo ya kawaida. Ortega ameongeza kusema kuwa ni uchaguzi utakaoleta Amani na usalama wa watu wa Nicaragua.