Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 10, 2023 Local time: 17:15

Mwanachama mkongwe ajiondoa chama tawala Tanzania


Kada mkongwe wa CCM Kingunge Ngomale-Mwiru
Kada mkongwe wa CCM Kingunge Ngomale-Mwiru

Mwanachama na kiongozi wa miaka mingi katika chama tawala cha Tanzania - CCM - Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru ametangaza kujitoa katika chama hicho kwa malalamiko kuwa hakifuati katiba.

Alitangaza hatua hiyo mjini Dar es salaam katika mkutano na waandishi wa habari akisema kuwa wakati huu wa utaratibu wa uchaguzi CCM imekiuka vibaya katiba yake.

Mzee Ngombale-Mwiru alionyesha wazi kumwunga mkono waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa katika juhudi zake za kuwania ugombea urais kupitia chama cha CCM.

Baada ya kung'olewa katika ugombea Lowassa aliondoka CCM na kujiunga na chama cha upinzani cha Chadema ambacho kilimpitisha kama mgombea urais na kukubaliwa na muungano wa vyama vya upinzani kuwa mgombea urais wa muungano wa Ukawa.

Tangu wakati huo Mzee Ngombale-Mwiru amekuwa wazi kulalamikia utaratibu uliotumiwa katika kupata mgombea wa CCM, akisema tangu mwaka 1995 utaratibu wa chama ulikuwa kuwaita wagombea wote na kuwahoji, lakini hilo halikufanyika mwaka huu.

Kwa miaka mingi ya utawala wa CCM Ngombale-Mwiru amekuwa kiongozi wa sera katika chama hicho. Alikuwa mtu wa karibu sana na mwasisi wa taifa Mwalimu Julius Nyerere katika uongozi wa chama cha CCM.

Katika mkutano wake na waandishi Ngombale-Mwiru alikiri kuwa uamuzi wake utawasumbua makada wenzake, wazee na vijana lakini alisema huu ni wakati wa mabadiliko.

Chama cha CCM hakijatoa tamko lolote kuhusu kuondoka kwa kiongozi huyo mkongwe.

XS
SM
MD
LG