Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:50

New Orleans ndio chimbuko la muziki wa Jazz Marekani


Eneo la River Board Walk katika mto Mississippi, New Orleans.
Eneo la River Board Walk katika mto Mississippi, New Orleans.

Jiji la New Orleans katika jimbo la Lousiana, kusini mwa Marekani ni jiji la kihistoria, mahala ambapo ulizaliwa muziki wa Jazz wa Marekani ambao unapendwa kote duniani.

Mji huo una wakazi wenye asili na makabila mbali mbali wakiwamo Wamarekani weusi, watu wenye asili ya Haiti , Wahindi na Wazungu.

New Orleans ina majina mengi ya Kifaransa na Kihispania kwa sababu kihistoria mji huo ulikaliwa na walowezi wa Kifaransa na baadaye Wahispania wakati wa ukoloni.

Vile vile mji huo unaojulikana kama “The Big Easy” au NOLA ikiwa na maana New Orleans, una vionjo vya staili ya ujenzi ulio tofauti na miji mingine ya Marekani kutokana na utamaduni wa walowezi hao wa Hispania na Ufaransa waliokaa mji huo miaka ya zamani.

Barabara nyingi za sehemu ya katikati ya mji huo ni ndogo na kutokana na hilo kunakuwa na foleni nyingi na kwa maana hiyo usafiri wa farasi pia hutumika na wa baiskeli za kubeba watu.

Mji huo unavutia watalii wengi kutoka kila pembe ya Marekani na duniani kwa ujumla.

Muziki katika mji wa New Orleans ni utamaduni mkubwa na umekuwepo kwa miaka mingi. Lakini ukiachilia mbali muziki wa kisasa watu wa mji huo wanapenda sana muziki wa kitamaduni, hasa wa tarumbeta na ule muziki wa Jazz na ngoma. Mjini humo mwezi wa nne kila mwaka kuna tamasha la muziki wa Jazz na mwezi wa nane kuna matamasha mengine mbali mbali ikiwamo lile lijulikanalo kamaRed Dress Run ambapo wakazi wa mji huo na wengine wengi wanavutwa kwenda kwenye mbio hizo ambazo hufanyika kila mwaka.

Angela amesafiri kutoka Nashville Tenesee mpaka New Orleans kwa ajili ya matembezi hayo.

“Mimi ni Angela kutoka Nashville Tennesee na nimekuja kusaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya mashirika ya hisani yapatayo 100 .” Hakika kabisa kuna zaidi ya watu 4000 na wamechangisha zaidi ya dola milioni 1.”

Katika mbio hizi washiriki waume kwa wake wanavaa magauni mekundu na kufanya matembezi ya kuchangisha fedha kwa masuala mbali mbali ikiwamo kusaidia wagonjwa wa kansa na wahitaji wengine mbali mbali kupitia vyama au taasisi za kutoa misaada.

Kuna familia nyingi za wahamiaji kutoka Haitina mmojawapo ni Jan Baptiste ambaye wazazi wake walihamia kutoka Haiti miaka kadhaa iliyopita na anaeleza wao ndio familia kubwa kuliko zote ya muziki huko New Orleans .

“Familia yetu ni ya kizazi cha Baptiste sisi ndio familia kubwa ya muziki kuliko zote hapa Luoisiana tuna kikundi chetu cha Baptiste na wanawe na Cango Square na tungependa watu duniani kote wangekuja na kutooa shukrani kwa New Orleans kwa yale tuliyowapa na pamoja na mababu zetu waliotupa muziki huu mzuri uitwao Jazz , kutoka muziki wa pili blues , Mardi Gras Indian, Funck,R&B , Wahindi weusi. Watu kutoka Morrocco, Ufaransa , Dominican Republic, Brazil, Ghana, Ivory Coast rudini kwenye asili yenu hapa New Orleans na sisi tutarudi kwenye asili yetu kwa mama Afrika.”

Mji huu pamoja na changamoto ya kupata athari za kimbunga cha Katrina mwaka 2005 unaendelea kukua na kuvutia wageni wengi kwa sauti za muziki na tarumbeta. Kinfoly ni mpiga tarumbeta mjini New Orleans

“Ni New Orleans hakuna kitu kinachotokea kama hiki popote duniani unaweza tu kupata muziki kama huu ikiwa utakuja New Orleans nimemaliza”.

Mji huu una mengi ya kimuziki kila unapopita mwishoni wa juma kuna maandamano ya aina fulani ya muziki wa Jazz ukitiwa nakshi na ngoma na matarumbeta au watu wanaotembea na spika kubwa la muziki likiwa limefungwa amplifaya na kupiga muziki mkubwa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Sunday Shomari, Washington, DC

XS
SM
MD
LG