Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 15, 2024 Local time: 08:23

Nchi tatu Afrika zaanza juhudi za nishati ya nuklia


Ramani inayoonesha nchi tatu barani Afrika zenye juhudi ya kuongeza nishati ya nuklia
Ramani inayoonesha nchi tatu barani Afrika zenye juhudi ya kuongeza nishati ya nuklia
Nchi tatu barani Afrika zimeanza juhudi za kuongeza nishati ya nuklia katika mikonga yao ya umeme. Kenya na Nigeria zinataka kuanza nishati ya nuklia wakati Afrika kusini – nchi pekee kusini mwa bara la Afrika ambayo ina mitambo ya nuklia – inataka kupanua uwezo wake. Mpaka sasa, mataifa ya Afrika yamekuwa yakitegemea mifumo ya kizamani kuzalisha umeme – nguvu za maji au mkaa wa mawe. Lakini vyanzo hivyo vimekuwa na madhara ya kijamii na mazingira, na hata kusababisha watu kuhama makazi yao. Lakini swali kubwa linaloulizwa ni jee Afrika ina uwezo wa kuanza nishati ya nuklia?

Kulingana na takwimu za Benki ya Dunia ni chini ya asilimia 10 tu ya jumla ya makazi yote ya watu barani Afrika ambayo yanapata umeme. Hali hiyo kwa namna kubwa inaathiri pia maendeleo ya viwanda na sekta nyinginezo katika bara masikini kuliko yote duniani.

Shida hiyo ya umeme ndio inasababisha baadhi ya nchi za Afrika kutafakari nishati ya nuklia – mfumo ambao unatumiwa katika baadhi ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea kama vile Marekani, India na China.

Kelvin Kemm, mtaalam wa fizikia ya nuklia huko Afrika Kusini, anasema Afrika inahitaji kuangalia nje ya mifumo ya uzalishaji umeme inayotumika sasa. Anasema “kwa jumla inapata umeme unaotokana na nguvu ya maji, na kila mtu anajua kuwa ukame wa miaka kadha barani humo unawezekana. Kwa hiyo ni hatari kujenga uchumi kwa kutegemea umeme unaotokana na maji.”
Matumizi ya nishati ya nuklia nchini Afrika kusini
Matumizi ya nishati ya nuklia nchini Afrika kusini


Afrika Kusini ni nchi pekee barani humo ambayo ilifanikiwa kutengeneza teknolojia ya nuklia, na iliwacha mpango wake wa silaha za nuklia katika miaka ya 90. Leo hii mtambo wa nuklia wa Koeberg unatoa karibu asilimia tano ya umeme wa nchi hiyo. Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma anasema anataka kuongeza uwezo wa umeme wa nuklia ili kupunguza kutegemea umeme unaotokana na mkaa wa mawe.

Kenya na Nigeria zinasema nazo zinaandaa mipango yao ya nuklia kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu. Mtaalam Kelvin Kemm anasema mahitaji ya umeme Afrika ni makubwa sana kiasi kwamba mifumo ya sasa ya uzalishaji umeme haiwezi kukidhi mahitaji hayo kama vile ambavyo nuklia ingeweza.

Wapinzani wa nishati ya nuklia wanasema teknolojia hiyo ina hatari zake, wakikumbusha ajali zilizotokea Fukushima, Japan au Chernobyl katika Soviet Union ya zamani. Lakini hata wapinzani hao wanahofu kwamba hatari hizo huenda zikafunikwa na ukweli kwamba mahitaji ya umeme ni makubwa mno.

Wataalam wanasema itachukua miaka, hata miongo kadha, kabla Afrika kupata namna ya kukidhi mahitaji ya umeme, ama kwa nishati ya nuklia au njia nyinginezo. Lakini kila mtu anakubali kuwa umeme zaidi unahitajika kuleta mwanga barani Afrika.
XS
SM
MD
LG