Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 22, 2024 Local time: 10:26

NATO kujadili operesheni ya Libya mjini London


Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen

Mkuu wa NATO atajadili operesheni za ushirika nchini Libya na viongozi wa Uingereza Jumatano, baada ya NATO kupiga malengo kadhaa katika mashambulizi mengine ya anga katika mji mkuu wa Libya kwa saa kadhaa.

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen anakutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na waziri wa mambo ya nje, William Hague mjini London.

Mapema wiki hii mkuu wa jeshi la majini la Uingereza alionya kwamba jeshi la Uingereza huwenda likashindwa kuhimili kiwango cha operesheni zake kwenye mwambao wa Libya kwa muda mrefu bila kupatiwa misaada.

Mashambulizi ya anga ya NATO yalipiga mji mkuu wa Libya, Tripoli Jumanne jioni baada ya kusitishwa kwa muda mfupi. Mashahidi wanasema walisikia milio mikubwa ya milipuko kati kati ya Tripoli na waliona wingu la moshi.
Vyombo vya habari vya serikali ya Libya vinasema mabomu yalipiga maeneo ya raia na kulikuwa na ripoti za vifo.

Mji mkuu wa Libya na maeneo yanayozunguka yamekuwa yakilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya anga ya NATO, tangu ushirika huo ulipoanza operesheni za kijeshi nchini Libya mwezi Machi. Waasi wa Libya wanajaribu kusonga mbele kuelekea Tripoli, huku ushirika ukifanya mashambulizi kwa majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya, Moammar Gadhafi.

Katika siku za karibuni waasi wamesonga mbele kutoka mji wa bandari wa Misrata kuelekea Tripoli na kuvunja uzio wa serikali. Vikosi kadhaa vya uasi vimeusukuma mstari wa mbele magharibi ktuoka Misrata hadi kwenye viunga vya Zlitan, mji jirani unaoshikiliwa na majeshi ya bwana Gadhafi.

XS
SM
MD
LG