Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, zimeahidi takriban dola milioni 151 kwa mfuko wa Umoja wa Umoja huo kwa ajili ya uimarishaji wa amani.
Wakati wa mkutano maalum ulioitishwa na baraza la Umoja wa Mataifa mjini New York, viongozi wa nchi na serikali za mataifa 26 walitoa ahadi hizo na baadhi yao kusema kwamba wanaunga mkono kwa dhati hazina hiyo.
Uchangishaji huo wa fedha ulifanyika kando mwa kikao cha baraza kuu, na hazina hiyo itasaidia kuboresha mikakati ya kutafuta amani katika kipindi cha mwaka 2017-2019.
Afisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, siku ya Alhamisi ilitoa taarifa kuwa fedha hizo zitatumika kwenye miradi mbalimbali katika nchi zaidi ya 20, ikiwa lengo kuu ni kudumisha amani na kuzuia migogoro.
Baadhi ya nchi zilizotoa michango yake ni pamoja na Kenya, Mexico, Uholanzi, Jamhuri ya Korea, Somalia, Sri Lanka, Sweden na Uingereza.
“Kwa jumla, kufikia sasa mfuko huo mfuko huo umepokea ahadi zinazofikia dola milioni 300 kwa miaka mitatu ijayo,” taarifa hiyo ilisema.
Naibu wa rais wa Kenya, William Ruto, aliiambia Sauti ya Amerika kuwa Kenya ilichanga dola milioni kumi kwenye hafla hiyo.
Wakati huo huo, huku mkutano mkuu wa baraza la Umoja wa Mataifa ukiingia siku yake ya nne, swala la mikakati ya kuwezesha wanawake kiuchumi lilijadiliwa kwa kina, ambapo jopo maalum la ngazi ya juu lililopatiwa jukumu la kutafiti na kuibuka na ripoti likiwasilisha ripoti yake ya kwanza kabia kwa Katibu mkuu Ban siku ya Alhamisi.
Video iliyochezwa kwenye ukumbi huo ilionyesha baadhi ya changamoto zinazowakabili wanawake ulimwenguni.
Winnie Byanyima, ambaye ni mmoja wa ni mmoja wa wajumbe wa jopo hilo, alisema kuwa uchumi wa dunia hautilii maanani sana mchango wa wanawake.
“Kimsingi kazi ya jopo hili haiwezi kufumbia macho uchumi ambao unawabagua wanawake na makundi mnengine ya watu maskini, uchumi ambao unashindwa kuthamini kazi ya wanawake," alisema.