Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, jana Jumatatu aliahidi kuendelea kutafuta suluhisho la amani kati ya mataifa mawili ya Israeli na Palestina, katika muda wa miezi tisa iliyosalia, kabla ya Rais Barak Obama kung’atuka mamlakani.
Katika hotuba yake kwa kundi la wanaharakati wa Israeli, J Street, Kerry alisisitiza umuhimu wa kumaliza mzozo wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili, na kusema kwamba njia ya pekee ya kupata suluhisho la kudumu, ni ile ya kutambua mwelekeo wa kuwepo kwa nchi mbili.
Kerry alisema na ninamnukuu: “Huwezi kuendelea kulaani upande moja au nyingine na ukose kujaribu kubadilisha maisha ya watu na kujenga uwezo wa kubadilisha mawazo.” Waziri Kerry alisema ni lazima wadau wote waongeze bidii ili kutafuta suluhisho kwa mzozo huo.