Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 01, 2023 Local time: 07:02

Mzozo kati ya mahakama na bunge waendelea nchini Kenya


Jaji mkuu Martha Koome alipokuwa katika kikao cha uthibitisho wake katika mahakama ya juu mjini Nairobi Kenya.
Jaji mkuu Martha Koome alipokuwa katika kikao cha uthibitisho wake katika mahakama ya juu mjini Nairobi Kenya.

Mzozo unaohusu idara za mahakama na bunge, unaendelea kutokota baada ya jaji mkuu Martha Koome kuliandikia bunge kudhibiti maafisa wa mahakama

Mzozo unaohusu idara mbili za serikali nchini Kenya, idara ya mahakama na bunge, unaendelea kutokota baada ya jaji mkuu Martha Koome kuliandikia bunge kudhibiti maafisa wa mahakama kufika mbele kamati ya bunge kuhusu uhasibu kuelezea suala la kuwapo maafisa wengi katika nafasi za ukaimu.

Spika wa bunge hilo Justin Muturi amekariri kuwa maafisa wa idara ya mahakama ni lazima wafike mbele ya bunge kuelezea matumizi ya fedha na masuala mengine yanayohitaji ufafanuzi zaidi la sivyo bunge halitaiwekea fedha idara ya mahakama.

Miezi miwili tu baada ya Jaji mkuu Martha Koome kuapishwa kuwa jaji mkuu wa Kenya wa 15 na mwanamke wa kwanza kuwahi kufanya hivyo katika historia ya Kenya, jaji huyo ameanza kuzungumza kwa ukakamavu kuhusu kuingiliwa kwa uhuru wa idara ya mahakama.

Japo Jaji Mkuu Martha Koome ameeleza kuwa ipo haja kuu ya matawi ya serikali bunge, idara ya mahakama na serikali kuu kufanya kazi kwa pamoja na kuondoa ushindani usiofaa, amekariri kuwa tawi moja halistahili kuonyesha jingine ubabe usiofaa, na iwapo hilo litafanyika basi hapatakuwepo na maelewano.

Koome ameeleza kuwa ataendeleza mafanikio yaliyowekwa na watangulizi wake na kuhakikisha uhuru wa mahakama unatiliwa mkazo zaidi.

Wiki iliyopita Jaji Mkuu kupitia barua kwa bunge Jaji mkuu Martha Koome, amedhibiti uwezekano wa Msajili Mkuu Ann Amadi ambaye ndiye mhasibu mkuu wa idara ya mahakama kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu Uhasibu kuelezea kwa nini pamekuwapo na idadi nyingi ya wafanyakazi wa idara hiyo katika nafasi za ukaimu waliohudumu kwa muda mwingi. Inaeleweka kuwa zaidi ya maafisa 10 wa idara ya mahakama wamehudumu kwa ukaimu kwa zaidi ya miaka kumi bila kuwapo kwa ishara kwamba wanaweza kuteuliwa katika nafasi hizo. Hii ilinukuliwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu katika ripoti yake ya ukaguzi wa idara ya mahakama ya 2018/19. Hili katika ripoti hiyo likitajwa kama linalokiuka Mwongozo wa Sera na Taratibu za Idara ya Mahakama.

Katika barua hiyo, Jaji Mkuu Koome anaeleza bunge kuwa mikakati yake ya kuwakagua maafisa wa Idara ya mahakama inajikita kwenye vitisho wala si suala la uelewa unaohitajika.

Hata hivyo, Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi ameeleza kuwa Jaji Mkuu Martha Koome hawezi kuwazuia maafisa wa mahakama kufika mbele ya kamati za uangalizi za Bunge.

Muturi anasisitiza kwamba Mahakama haiwezi kutolewa kwa jukumu la kikatiba la ukaguzi wa bunge.

Aidha, amekariri kuwa wote wanaotakiwa kufika mbele ya kamati za bunge ni sharti wafanye hivyo la sivyo washtakiwe kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Mabunge duniani kote yana katiba ya kusimamia ngazi zote za serikali. Katika utendaji wa kazi yake ya usimamizi, bunge lolote hutegemea sana ripoti ambazo zinatoka kwa ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali. Wakati wa kutekeleza agizo lake, bunge halina budi kufuata sheria” anasema Spika Muturi.

Vile vile, Spika Muturi anaeleza wanahabari kuwa katazo la Jaji Mkuu Martha Koome kumzuia Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Ann Amadi kufika mbele ya kamati ya bunge ya Uhasibu kuelezea ni kwa nini imeshindwa kuajiri mkurugenzi wa fedha baada ya kipindi cha miaka saba kunaweza kuiifanya idara hiyo kushtakiwa kwa matumizi mabaya ya bejeti ya mahakama.

"Ikiwa wanatoka katika Mahakama, na ni watu wanaopaswa kufahamu kanuni zinazomtaka mtu kusilikizwa kwanza kabla kuhukumiwa lakini ikiwa watashindwa kuonekana kwa makusudi, basi hawapaswi kulaumu bunge kwa kutoa mapendekezo yoyote ambayo bunge linaweza kutoa” Spika Muturi ameongezea.

Spika Muturi vile vile ameonya kuwa bunge litakuwa na uhuru miongoni mwa mambo mengine kuzuia ufadhili kwa maafisa wa mahakama wanaoonesha mazoea ya kutowajibikia matumizi ya fedha za umma.

Na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika Nairobi.

XS
SM
MD
LG