Mwili wa bingwa wa ndondi duniani, Muhammad Ali uliwasili katika makazi yake kwenye mji wa Louisville katika jimbo la Kentucky siku ya Jumapili.
Ali alifariki Ijumaa akiwa na umri wa miaka 74 kutokana na matatizo yanayohusiana na ugonjwa wa Parkinson. Msafara kuelekea nyumba ya kuhifadhia maiti uliongozwa na gari lililobeba jeneza ambalo liliwasili kwa ndege ya kukodi ambayo iliubeba mwili wa Ali kutoka Arizona mahala ambako mauti yalimfika.
Wakazi wa Louisville watampa heshima ya kumuaga kote mjini humo siku ya Ijumaa ikifuatiwa na mazishi ya umma kwenye uwanja wa michezo.
Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton ni miongoni mwa wageni waliopangiwa kuzungumza.