Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 00:46

Mwenyekiti wa IEBC: Mahakama imeniondolea lawama zote


Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Wafula Chebukati wakati akitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais Agosti 15 2022. PICHA: Reuters
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Wafula Chebukati wakati akitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais Agosti 15 2022. PICHA: Reuters

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka ya Kenya IEBC Wafula Chebukati amesema kwamba uamuzi wa Mahakama ya Juu nchini humo wa kuidhinisha matokeo ya kura ya urais ambayo yalimtangaza William Ruto kuwa mshindi umemuondolea lawama.

Baada ya majaji wa mahakama ya juu nchini Kenya, kwa sauti moja wametupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Raila Odinga na wengine kupinga ushindi wa William Ruto uliotangazwa na IEBC, mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati ameeleza kuwa hatua hiyo ya mahakama imemuondolea shutuma za kuboronga uchaguzi huo.

Chebukati wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, ameeleza kuwa licha ya maafisa wa tume hiyo kupitia mateso, vitisho na visa vya kutekwa nyara, tume hiyo imesimama kidete na kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Aidha, ameeleza kuwa uchaguzi ni mchakato wala si tukio la siku moja na kukariri kuwa uamuzi wa mahakama ni ushahidi wa kutosha kuwa tume hiyo imeandaa uchaguzi huru, wa haki, wazi na wa kuaminika ambao ulitimiza matakwa ya kidemokrasia kwa raia wa Kenya.

Jopo la majaji 7 wamekubaliana kwamba uchaguzi ulikuwa huru na haki

Majaji saba wa mahakama ya juu, wote kwa kauli moja wameamuru kuwa uchaguzi wa Kenya wa urais wa Agosti 9 umeafiki viwango vya kisheria na kwamba Dr. William Ruto, alitangazwa inavyostahili kwa kupata kura asilimia 50%+1 ya kura zote zilizopigwa, huku ikikariri kuwa teknolojia iliyotumiwa na IEBC ilikidhi viwango vya uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi ili kuhakikisha matokeo sahihi na yanayoweza kuthibitishwa.

Mahakama hiyo imeeleza kuwa mwenyekiti wa tume ya IEBC Wafula Chebukati hastahili kujilimbikizia majukumu ya kuendesha mchakato wa kuthibitisha matokeo ya kura ya urais, lakini hatua za mwisho mwisho za makamishna wanne waliopinga matokeo hayo, ni za kutiliwa shaka.

Kenyatta ahutubia taifa kupitia you tube

Rais Uhuru Kenyatta, katika hotuba iliyorekodiwa, kwa taifa, ameeleza kuwa serikali yake itawezesha kipindi cha mpito kwa njia rahisi ilivyo kisheria, kukabidhi madaraka kwa utawala unaokuja.

Kenyatta hata hivyo amewataka wakenya kuwa macho na kuwawajibisha majaji kwa maamuzi yao.

Bila kumtaja naibu wake kwa hotuba hiyo, kando na kuwataka Wakenya wote kuheshimu taasisi zinazowalea viongozi wapya, ameeleza kuwa anawatakia heri viongozi wote waliochaguliwa, lakini anawataka kuwajibikia maslahi ya umma.

Hesabu za IEBC mwaka 2022

Mnamo Agosti 15, 2022, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Dr. William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa kupata kura milioni 7.81 ikiwa ni asilimia 50.49 na Odinga akiwa na kura milioni 6.94 ikiwa ni asilimia 48.85.

Odinga alipinga matokeo hayo katika mahakama kuu.

Mahakama imetupilia mbali kesi hiyo Septemba 5 2022 kwa kukosa ushahidi.

Chebukati amewaambia waandishi wa habari kwamba mfumo wa uchaguzi wa digitali wa IEBC ulifanyiwa majaribio kwa muda wa miaka 5 ili kuhakikisha kwamba uchaguzi wa mwaka 2022 unakuwa huru na haki.

“Tulianza kutayarisha mfumo huu punde baada ya uchaguzi wa mwaka 2017 na tulifanyia majaribio ya kila mara na kuutumia katika zaidi ya chaguzi ndogo 40,” amesema Chebukati.

Waliohusika na mauaji ya afisa wa IEBC waajibishwe

Tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC inataka wahusika wote katika dhuluma, kushambulia na mauaji ya maafisa wake, wakamatwe na kushitakiwa.

Afisa wa IEBC Daniel Musyoka alitekwa nyara akiwa kazini na baadaye kupatikana akiwa ameuawa.

Ghasia pia zilitokea kwenye ukumbi wa kuhesabu na kuhakiki kura za urais wa Bomas, wanasiasa wakiwashambulia makamishna wa IEBC, mda mfupi kabla ya matokeo ya urais kutanganzwa. Makamishna wa IEBC waliripotiwa kujeruhiwa.

"Hakuna mtu yeyote amekamatwa kufikia sasa kwa kushambulia wafanyakazi wa IEBC. Hakuna hata shirika la kutetea haki za kibinadamu limeshutumu mashambulizi na mauaji hayo. Kufanya kazi na tume ya uchaguzi haistahili kuwa hukumu ya kifo,” amesema Chebukati.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi.

XS
SM
MD
LG