Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Januari 30, 2023 Local time: 21:28

Mwanasheria Mkuu Nigeria awaondolea lawama maafisa wa usalama katika mauaji ya waandamanaji


Mwanasheria mkuu nchini Nigeria amesema kwamba watu waliowapiga risasi na kuua waandamanaji nchini humo hawajulikani na kwamba huenda watu waliofunika nyuso zao na kuvalia sare za kijeshi ndio waliohusika.

Abubakar Malami amesema kwamba ni mapema sana kusema iwapo polisi walihusika katika tendo la kuwapiga risasi waandamanaji waliokuwa wanalalamikia vitendo vya polisi kutumia nguvu kuzidi kiasi.

Maandamano kote nchini Nigeria yaligeuka na kuwa vurugu Oktoba 20 baada ya kuripotiwa kwamba wanajeshi walikuwa wamewapiga risasi baadhi ya waandamanaji mjini Lagos, muda mfupi baada ya kuwekwa masharti ya watu kusalia nyumbani saa 24.

Wanajeshi na polisi wanaripotiwa kuua watu 12 katika mitaa miwili ya Lagos Oktoba 20, kulingana na walioshuhudia pamoja na shirika la Amnesty International.

Polisi na wanajeshi wamekanusha madai hayo.

Mwanasheria Mkuu Abubakar Malami amewaambia waandishi wa habari mjini Lagos kwamba uchunguzi unaendelea na kwamba kuna haja kujua iwapo kweli kuna watu walipigwa risasi na kwamba kama tukio hilo lilitokea, na kama waliohusika walikuwa wanajeshi.

“Huwezi kufutilia mbali uwezekano wa wahalifu kuhusika katika tukio hilo,” amesema Malami katika kikao na waandishi wa habari ambacho pia kilihudhuriwa na maafisa kadhaa wa serikali wakiwemo mawaziri wa ulinzi na fedha.

Jimbo la Lagos limeamuru uchunguzi wa kina kufanyika.

Wiki iliyopita, jeshi lilisema kwamba serikali ya jimbo la Lagos iliomba jeshi kuingilia kati na kurejesha utulivu wakati wa maandamano, lakini wanajeshi hawakuhusika katika kupiga raia risasi.

Maandamano makubwa ya nchi nzima yalitokea Nigeria kupinga polisi kutumia nguvu kuzidi kiasi mnamo mwezi uliopita.

Maandamano hayo yametajwa kuwa mabaya zaidi tangu kurejea kwa utawala wa kiraia mwaka 1999.

Wiki iliyopita, Polisi wa Nigeria wamesema kwamba maafisa wake wamefariki katika machafuko hayo na vituo vya polisi 205 kuharibiwa.

Maandamano hayo ambayo yamemalizika, ndio yamekuwa mtihani mkubwa kwa utawala wa rais Muhammadu Buhari tangu alipoingia madarakani mwaka 2015.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG