Mwanajeshi huyo aliyeuawa na majeruhi wote ni kutoka kikosi cha Jordan, afisa mmoja wa usalama amesema kwa masharti ya kutotajwa jina.
Msafara huo ulishambuliwa kwa silaha ndogo ndogo na maguruneti ya roketi katika shambulio lililodumu karibu saa moja, msemaji wa MINUSMA Olivier Salgado aliandika kwenye Twitter.
“Kwa bahati mbaya, mmoja wa wanajeshi hao wa Umoja wa mataifa alifariki kutokana na majeraha aliyopata kufuatia shambulio hilo,” Salgado amesema.
Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu wanaoshukiwa kufanya shambulio hilo.
Katika taarifa, mwakilishi maalum wa Umoja wa mataifa nchini Mali na mkuu wa MINUSMA, El Ghassim Wane, amesema walinda amani hao waliwazuia washambuliaji ambao waliokuwa na silaha nzito.
“Ninalaani vikali shambulio hili, ambalo ni jaribio jingine la kukata tamaa la makundi ya kigaidi kukwamisha harakati za kutafuta amani nchini Mali na utekelezaji wa mamlaka ya MINUSMA,” amesema.
Shambulio hilo ni tukio la tano kutokea katika jimbo la Kidal katika kipindi cha wiki moja, taarifa ya MINUSMA imesema.