Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 19:02

MV Nyerere : Miili 116 yatambuliwa, vifo ni zaidi ya 150


Waokoaji waopoa miili zaidi kutoka eneo la majini la kisiwa cha Ukara, katika Ziwa Victoria Septemba. 21, 2018.
Waokoaji waopoa miili zaidi kutoka eneo la majini la kisiwa cha Ukara, katika Ziwa Victoria Septemba. 21, 2018.

Miili 116 kati ya 151 iliyo opolewa baada ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere juzi Septemba 20, 2018 imetambuliwa na ndugu wa familia zao.

Idadi hii imeripotiwa na vyombo vya habari ikiwemo gazeti la Mwananchi,

Ripoti zaidi zinasema kuwa ndugu, jamaa na wananchi wamepiga kambi eneo la bandari ya Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe tangu kazi ya uokoaji ilipoanza.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi Septemba 22, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema Serikali itatoa ubani wa 500, 000/- kwa familia, kwa kila maiti itakayo tambuliwa na kuchukuliwa kwa ajili ya maziko.

Tangu Jumamosi asubuhi, miili 30 imeopolewa na kufanya idadi ya miili iliyoopolewa hadi sasa kufikia 166 baada ya mili mingine 136 kuopolewa hadi Ijumaa jioni.

Miili yote iliyoopolewa imehifadhiwa katika Kituo cha afya cha Bwisya.

Siku ya Ijumaa Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania alitangaza siku 4 za maombolezo kuanzia kufuatia ajali ya Ferri ya MV Nyerere iliyozama katika ziwa Victoria siku ya Alhamisi.

Katika ajali hiyo, watu zaidi ya 130 wamethibitishwa kupoteza maisha kufikia Ijumaa, huku wengine zaidi ya 40 wakiwa tayari wamesha okolewa. Serikali imesema zoezi hilo la uokoaji linaendelea.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba mizigo na abiria wengi zaidi ya uwezo wake. Serikali tayari imetuma wachunguzi katika eneo la tukio la ajali hiyo kufanya uchunguzi wa kina.

Rais Magufuli ameagiza watendaji wa Kivuko na wengine wote wakamatwe katika hali ya uchunguzi huo, akiwemo kapteni wa meli hiyo.

Shirika la habari la Reuters liliwanukuu maafisa wa serikali ya Tanzania wakisema kuwa wanahofia huenda watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha katika ajali hiyo.

Maafisa wa usafiri wanasema Ferry ya MV Nyerere inauwezo wa kuchukua abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu.

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda waliohojiwa na vyombo vya habari vya Tanzania walisema kwamba wakati wa ajali hiyo, feri hiyo ilikuwa imebeba watu wengi kupita kiasi.

Ijumaa usiku, maafisa wa serikali ya Tanzania walisema huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.

Feri hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa watu wa Ukerewe tangu 2004.

XS
SM
MD
LG