Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 10:39

Museveni: Sitaki mafuta ya Russia, sitaki kujiingiza katika mgogoro na Marekani


Rais wa Uganda Yoweri Museveni. PICHA: AP
Rais wa Uganda Yoweri Museveni. PICHA: AP

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kwamba nchi yake haitaagiza mafuta kutoka Russia kama alivyoomba waziri wa mambo ya nje wa Russia, Sergey Lavrov wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Uganda.

Katika hotuba yake kwa taifa, Museveni amesema kwamba licha ya Russia kutaka kuiuzia Uganda mafuta kwa bei rahisi, na licha ya kwamba bei ya mafuta imeongezeka sana nchini Uganda, hataki “kujiingiza katika mgogoro kati ya Marekani na Russia.”

Amesema kwamba “serikali itatafuta mbinu mbadala za kuhakikisha kwamba kuna mafuta ya kutosha nchini Uganda, wakati inajitayarisha kutekeleza mikakati ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuwa na nishati safi, magari na pikipiki zinazotumia nguvu za umeme.”

“Endapo tutanunua mafuta kwa bei rahisi kutoka Russia, ina maana kwamba tunakiuka vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya Russia.” Amesema Museveni, akiongezea kwamba “tangu tatizo lilipoanza, nimekuwa nikiwasiliana na viongozi wa Russia na Marekani. Sasa mnaweza kuona mazungumzo yetu yameanza kuruhusu nafaka na ngano kusafirishwa kutoka Ukraine.”

“Sitaki kujiingia katika mgogoro usionihusu moja kwa moja”

Museveni amesisitiza kwamba njia ya kusuluhsisha uhaba wa bidhaa muhimu unaoshuhudiwa duniani kwa sasa ni kutumia diplomasia.

“Kama nataka kununua mafuta, ningeiambia Russia kusafirisha mafuta hayo hadi hapa na wangefanya hivyo. Lakini hatua hiyo inatuweka katika matatizo na Marekani ambayo sio jambo zuri. Kwa sasa, tutumie vizuri mafuta tuliyo nayo huku tukitafuta mbinu mbadala.”

Hotuba ya Museveni kwa taifa imejiri siku chache baada ya kukutana na mabalozi wa ngazi ya juu wa Russia na Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov alikuwa Uganda Julai 26. Alisema kwamba “Russia ilikuwa tayari kufanya mazungumzo na Uganda, kuhakikisha kwamba Uganda inapata mafuta ya bei rahisi au nafuu ili kukabiliana na uhaba wa bidhaa hiyo nchini humo.”

Waziri wa mambo ya nje wa Russia aliahidi Uganda mafuta kwa bei nafuu

Lavrov alisema kwamba “tunauza mafuta kwa nchi zote ambazo zinataka na hakuna vizuizi vya aina yoyote kwa nchi yoyote inayotaka kununua mafuta, iwe India, taifa lolote la Afrika.”

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas Greenfield amekuwa nchini Uganda mwishoni mwa wiki na kufanya mazungumzo na rais Yoweri Museveni. Balozi huyo alimtahadharisha Museveni dhidi ya kufanya biashara ya mafuta na Russia.

“Kuhusu vikwazo dhidi ya Russia, kwa mfano uuzaji wa mafuta, iwapo nchi inaamua kufanya bishara hiyo na Russia, au kuhusu biashara ambazo zimewekewa vikwazo, basi inavunja vikwazo,” amesema Linda katika kikao na waandishi wa habari akiwa Kampala, Uganda.

Museveni anataka nchi za Afrika zisihusishwe na vikwazo dhidi ya Russia

Museveni hata hivyo ameiomba Marekani kuondoa nchi za Afrika kwenye masharti hayo kwa sababu “zinaendelea kuathirika sana kutokana na gharama ya juu ya Maisha.”

“Kama unataka kuzisaidia nchi zinazoendelea, mbona msiziondoe nchi hizi kwenye vikwazo hivyo vinavyotokana na mgogoro ambao hazihusiki kabisa. Swala muhimu hapa linahusu bei ya juu ya mafuta ambayo inaendelea kusababisha bei za bidhaa kupanda kutokana na gharama ya juu ya usafiri.” Amesema Museveni.

Thomas-Greenfield amesema kwamba alikuwa amepanga kutembelea Uganda kabla ya waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov kutembelea nchi hiyo na kwamba ziara ya Lavrov ilikuwa ya “kumshawishi Museveni kuunga mkono Russia.”

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG