Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 02, 2022 Local time: 08:29

Museveni atishia kutumia nguvu zote dhidi ya wanaosumbua wafuasi wake


Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametishia kutumia nguvu zote kukabiliana na wanasiasa wa upinzani aliosema wanatishia wafuasi wake wa chama cha National Resistance Movement (NRM).

Museveni amesema kwamba atatumia mbinu zote kuwanyamazisha wapinzani wake wanaomsumbua, kutishia wafuasi wake na kutishia amani ya Uganda. Amesema hayo wakati polisi walikuwa wanakabiliana na mgombea wa urais Patrick Amuriat, pamoja na kumkamata wakili maarufu wa kutetea haki za kibinadamu.

Akizungumza katika lugha ya kiganda akiwa katika kampeni katikati mwa Uganda, Museveni amedai kwamba wanasiasa wa upinzani wanawahangaisha wafuasi wake kote nchini na kuwalazimisha kuwaunga mkono.

Amesema usumbufu huo hauwezi kukubalika kamwe, akiongezea kwamba atakayejaribu kuwapiga, kuwalazimisha wafuasi wake, au kuzuia wafuasi wake kufanya wanachotaka kumuunga mkono, atakutana na hasira yake.

Ametishia kutumia nguvu zote kukabiliana na wanasiasa wa upinzani aliosema lengo lao kuu ni kufanya vurugu, akisema kwamba nguvu kama zilizotumika kuzima maandamano yaliyotokea wakati polisi walipomkamata mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, zitatumika tena. Watu 54 walikufa wakati wa maandamano hayo, wengi wao walipigwa risasi na polisi. Watu kadhaa pia walikamatwa.

“Wanasema kwamba watawapiga wafuasi wangu. Hutampiga mtu yeyote na huwezi kumpiga mtu yeyote. Waliojaribu kufanya vurugu jijini Kampala, wanajua kilichowafikia. Huwezi kuwatishia wala kuwapiga wafuasi wa NRM. Unatafuta matatizo makubwa.” Amesema Museveni

Wagombea wa NRM waelezea ugumu katika kampeni dhidi ya Bobi Wine

Viongozi wa chama cha NRM katikati mwa Uganda, wamemuambia Museveni kwamba imekuwa vigumu kufanya kampeni katika sehemu hiyo kwa sababu ya ufuasi mkubwa anaopata Bobi Wine, na kuomba msaada wa Museveni kutumia kila mbinu kukabiliana na ufuasi huo.

“Hii sehemu inahitaji kuangaziwa zaidi ili kukabiliana na upinzani unaoongozwa na Bobi Wine. Tunaomba msaada wa haraka. Tunakuomba sana rais, utusaidie sana kukabiliana na upinzani ambao umeota mizizi hapa.” Amesema mgombea wa eneo bunge la Butambala Mafumo Kyeswa.

Museveni ameelekeza wafuasi wa chama chake cha NRM, maafisa wa chama hicho na viongozi wa ulaya kurekodi ushahidi wa wanasiasa wa upinzani wanaotishia wafuasi wake. Amesisitiza kwamba wanaofanya hivyo dhidi ya wafuasi wa NRM, hatawahi kurudia maisha yao yote.

“Hata huna ruhusa ya kunitisha wala kuninyooshea kidole. Kwa nini ufanye hivyo? Ukifanya hivyo unatafuta shida kubwa kutoka kwangu. Mimi huwa nawabembeleza watu, nakuwa muungwana na kuongea na watu vizuri. Nawabembeleza hata wanaofanya makosa. Halafu wewe uje kunitishia? Utajuta.” Amesema Museveni.

Wapinzani wa Museveni wasema wanahangaishwa sana na polisi

Matamshi ya Museveni yanajiri wakati wapinzani wake katika kugombea urais katika uchaguzi wa Januari 14 mwaka ujao, wanaendelea kumkosoa Museveni na wafuasi wake kwa kutumia polisi na wanajeshi kuvunja mikutano yao na picha zao kuharibiwa.

Polisi wametumia nguvu kuvunja mkutano wa mgombea wa chama cha Forum for democratic change Patrick Amuriat, wilayani Kabarole. Gen Mugisha Muntu na Gene Henry Tumukunde, wamekuwa wakilalamika kile wamekitaja kama polisi kutumiwa kuvuruga kampeni na kusema wanapendelea pande mmoja katika kampeni.

Wakili maarufu wa haki za kibinadamu akamatwa

Wakati huo huo, polisi wamemkamata wakili maarufu wa kutetea haki za kibinadamu nchini Uganda, na anayeteteza mashirika yasiyo ya kiserikali nchini humo, Nicholas Opiyo.

Bila kutoa maelezo zaidi, taarifa fupi ya polisi imethibitisha kukamatwa kwake na kusema kwamba anachunguzwa kuhusiana na utakatishaji wa fedha. Kukamatwa kwake kunajiri siku chache baada ya serikali ya Ugand akufunga akaunti kadhaa za benki za masharika yasiyo ya kiserikali, yakishutumiwa kwa kufadhili kampeni za wagombea wa upinzani, na ugaidi.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG