Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 09:49

Museveni ashinda uchaguzi wa rais Uganda, upinzani unadai ni wizi


Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni

Tume ya Uchaguzi nchini Uganda, ilitangaza Jumamosi kwamba Rais Yoweri Museveni ameshinda kura ya urais baada ya kupata kura 5,851,037 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, aliyezoa kura 3,475,298.

Hii ina maana kwamba Museveni, ambaye amekuwa rais wa nchi hiyo tangu mwaka wa 1986, ataongoza kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Museveni alipata asili mia 58.64 ya kura zote zilzizopigwa huku Wine akipata asili mia 34.83, kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Simon Byabakama.

Huu utakuwa muhula wa sita wa Museveni kufuatia vuta nikuvute ambayo imepelekea kampeni zilizokumbwa na maafa, ghasia na vurugu za kila aina.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi amesema kwamba jumla ya kura 10,359,479 zilipigwa, huku 381,386 zikiharibika.

"Hatukushinikizwa wala kazi yetu haikuingiliwa na mtu yeyote," alisema Byabakama akijibu maswali kutoka kwa waandaishi wa habari kwenye kituo kikuu cha tume hiyo katika eneo la Kyambogo.

Kyagulanyi amepinga matokeo hayo.

Afisa wa polisi wa Uganda anaonekana hapa akilinda sanduku la kupigia kura.
Afisa wa polisi wa Uganda anaonekana hapa akilinda sanduku la kupigia kura.

Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na wagombea 11 wa urais, mmoja akiwa mwanamke.

Mgombea kwa tikiti ya chama cha Forum for Democratic Change (FDC) Amuriat Oboi alikuwa wa tatu, akipata kura 323,536 ambazo ni asili mia 3.24 ya kura zote zilizopigwa.

Mugisha Muntu wa ANT alipata kura 65,334 huku mgombea kwa tikiti ya chama cha DP, Norbert Mao, akipata kura 55,665.

Wengine walikuwa ni John Kabuleta: 44,300, Nancy Kalembe: 37,469, John Katumba: 35,983, Willy Mayambala: 14,657, Fred Mwesigye: 24,673 na Henry Tumukunde, aliyepata kura 50,141.

Rais Yoweri Museveni Kaguta na mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
Rais Yoweri Museveni Kaguta na mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Baadhi ya wachambuzi waliozungumza na Sauti ya Amerika wamesema ushindi wa Rais Museveni ulitarajiwa.

"Inaonekana muda haujafika wa kumpeleka kijana Ikulu," alisema Bi Aida Mutenyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kabale.

Kyagulanyi, ambaye pia ni mbunge na msanii, alionekeana na wengi kama ambaye angetishia utawala wa muda mrefu wa Museveni hususan kutokana na kushuhudiwa kwa ufuasi mkubwa wa vijana.

Haikufahamika mara moja ni hatua zipi mwanasiasa huyo atakazochukua, baada ya kudai kuwa kura zake zimeibwa.

Kwa mujibu wa katiba ya Uganda, anayepinga matokeo ya uchaguzi ana muda wa siku 15 kuwasilisha malalamishi mahakamani.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG