Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 06:01

Museveni apuuza kilio cha wafanyakazi Uganda


Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Wafanyakazi nchini Uganda wameachwa na mshangao mkubwa baada ya Rais Yoweri Museveni kukataa kusikiliza kilio chao katika sherehe za kuadhimisha siku ya Kazi Duniani.

Katika hotuba yake Rais ameonyesha kupuuza ombi la wafanyakazi nchini la kutaka kuongezewa mishahara kwa kuwa gharama za maisha zimepanda kutokana na mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa katika sherehe hizo zilizofanyika Wilaya ya Palisa Mkoa wa Mashariki ya Uganda.

Museveni pia amekaidi msukumo wa vongozi wa wafanyakazi wa kutaka kiwango cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi kupandishwa kutoka dola mbili kwa sasa, na badala yake kutaka sheria kuundwa kuwanasa walevi na wacheza kamari.

Kutokana na kutokuwepo sheria ya kuwabana waajiri wafanyakazi nchini Uganda wamelalamika kuwa kila mwajiri anakuwa na hiari ya kulipa kiwango cha mshahara anachotaka.

Viongozi wa wafanyakazi wamesema kuwa sheria iliopo ya mwaka 1984 imeweka kiwango cha chini cha mshahara nchini Uganda kuwa ni Shilingi 6000 ambazo ni chini ya dola 2 za Kimarekani.

Mwenyekiti wa muungano wa wafanyakazi nchini Uganda Wilson Owere amemlalamikia Rais Yoweri Museveni wakati wa sherehe hizo akisema: “Haiwezekani kwa binadamu kupokea dola 2 kama mshahara. Zamani walikuwa wanalipa shilingi za Uganda 6,000 na mpaka leo hivi hakuna kiwango cha chini.”

“Watu wanawafanyisha kazi wafanyakazi na kuwapa wafanyakazi kile wanachokitaka kwa sababu hakuna sheria,” amesema mwenyekiti huyo.

Lakini Rais Museveni amewaambia wafanyakazi katika hotuba yake ya siku ya Wafanyakazi Duniani “adui yenu ni hawa wafanyakazi wa umma ambao ndio mafisadi wanao wazuilia kupata ajira." “Mimi nalenge kubuni nafasi za ajira milioni 15,” amesema.

Lakini muungano wa wafanyakazi nchini Uganda wamelaumu sera za uwekezaji Uganda kwa kuwahusisha wawekezaji kwa vitendo vya dhulma, na wanawatumikisha wafanyakazi masaa mengi zaidi kuliko vile inavyotakikana bila `ya malipo yoyote.

“Tukijaribu kuwaunganisha wafanyakazi wawekezaji wanakimbilia kwa rais kulalamika,” wamesema viongozi hao.

XS
SM
MD
LG