Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 02, 2022 Local time: 10:22

Museveni amteua mwanawe kuwa kamanda wa kikosi maalum cha jeshi


Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mkuu wa kikosi maalum SFC

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemteua mwanawe wa kiume Lt Gen Muhoozi Kainerugaba kuwa kamanda wa kikosi maalum cha jeshi SFC.

Muhoozi, mwenye umri wa miaka 46, pia ni mshauri maalum war ais, nafasi ambayo aliteuliwa mwaka 2017.

Uteuzi huo unafuatia mabadiliko ambayo rais Museveni amefanya Jumatano, katika uongozi wa jeshi la Uganda UPFD pamoja na katika jeshi la polisi.

Kikosi cha SFC kina majukumu ya kumlinda rais wa Uganda na kusimamia majukumu mengine ya kipekee kulingana na amri za kamanda mkuu wa jeshi ambaye ni rais Yoweri Museveni.

Muhoozi anachukua nafasi ya kamanda wa kikosi hicho kutoka kwa Maj. Gen. James Birungi.

Lt. Gen Muhoozi Kainerugaba, aliwahi kuwa kamanda wa kikosi hicho hadi mwaka 2017. Wakati huo, kulikuwa na madai kutoka kwa baadhi ya makamanda katika jeshi kwamba Museveni alikuwa anamtayarisha mtoto huyo wake wa kiume kumrithi.

Katika mabadiliko hayo ya Museveni, Maj Gen. Paul Lokech ambaye amekuwa Sudan kusini kwa majukumu maalum kwa ajili ya utekelezaji wa mkataba wa amani, ameteuliwa kama naibu wa mkuu wa polisi wa Uganda.

Maj Gen. Muzeeyi Sabiiti amefutwa kazi kama naibu mkuu wa polisi.

Mabadiliko baada ya maandamano yaliyosababisha vifo

Mabadiliko hayo yanajiri siku chache baada ya maandamano yaliyotokea katika sehemu mbalimbali za Uganda kufuatia hatua ya kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.

Polisi na wanajeshi walikabiliana na waandamanaji kwa nguvu, wakitumia risasi na gesi ya kutoa machozi. Zaidi ya watu 37 walipoteza maisha.

Museveni amesema kwamba mabadiliko aliyofanya yanalenga kuimarisha nguvu za maafisa wa usalama katika kukabiliana na maandamano ya kiraia.

“Polisi wanastahili kuwa na nguvu za kufanya kazi yao ipasavyo na kukabiliana na visa vya uvunjifu wa sheria, vitisho dhidi ya maisha ya wat una kulinda mali. Polisi yeyote asitetekeleza wajibu wake lazima aondolewe. Kuna maelfu ya watu wanaotaka kazi hiyo.” Amesema Museveni.

Ameendelea kusema kwamba anajivunia utendakazi wa jeshi la Uganda UPDF, hasa “walipokabiliana vilivyo na wasaliti wanaoungwa mkono na watu katika nchi za nje wiki chache zilizopita.”

Marekani yasema yafuatilia hali ya Uganda

Mjadala umekuwa ukiendelea nchini Uganda baada ya Marekani kutaka nchi hiyo kuandaa uchaguzi huru na haki Pamoja na kuheshimu haki za kibinadamu.

Uganda inajitayarisha kuandaa uchaguzi mkuu Januari tarehe 14 2021.

Katika ujumbe wa twiter alhamisi wiki iliyopita, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema kwamba “Marekani ni mshirika wa muda mrefu wa Uganda. Tunatarajia washirika wetu kutekeleza wajibu wao na kuandaa uchaguzi ulio huru na haki. Tunafuatilia kwa karibu sana matendo ya watu binafsi katika serikali ya Uganda kwa kutaka kujua anayetaka kuhujumu uchaguzi huo.”

Pompeo aliandika ujumbe huo wa twiter, saa chache baada ya mwenyekiti wa kamati ya maswala ya kimataida katika bunge la Marekani Eliot Engel, kutaka serikali ya Marekani kuwawekea vikwazo maafisa kadhaa wa usalama nchini Uganda kutokana na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu nchini Uganda.

Engel anataka utawala war ais Trump kuwawekea vikwazo kamanda wa jeshi nan chi kavu Generali Peter Elwelu, Generali James Birungi ambaye ameondolewa kama kamanda wa kikosi maalum cha jeshi SFC na mkuu wa ujasusi Generali Abel Kandiho.

Gen Elweelu aliongoza mashambulizi dhidi ya ufalme wa Rwenzuru wilayani Kasese mnamo mwaka 2016, yaliyopelekea vifo vya zaidi ya watu 100.

Wengine ni Maj Gen. Sabiiti Muzeyi ambaye ametimuliwa kutoka kwa nafasi ya naibu wa mkuu wa polisi na Col Chris Serunjogi Ddamulira ambaye ni kiongozi wa ujasusi katika jeshi la polisi.

Museveni asema hayupo tayari kuondoka madarakani

Katika mikutano yake ya kampeni, Museveni amewataja wapinzani wake kuwa maadui wa Uganda.

Siku chache zilizopita, Museveni amesema kwamba ataondoka madarakani pale atakuwa na uhakika kwamba kuna mtu mwenye uwezo wa kuongoza Uganda, anayeweza kuachia nchi.

Aliwataja baadhi ya wapinzani wake wakuu (Lt. Gen Henry Tumukunde ambaye alikuwa waziri wa usalama na aliyekuwa kamanda mkuu wa jeshi Maj. Gen. Mugisha Muntu) kuwa watu wazembe wanaotaka kusukumwa kama mkokoteni ndipo wafanye kazi.

Amesema kwamba wanaosema kwamba aondoke madarakani huwa wanamkasirisha sana lakini mara nyingi ameamua kuwa mtulivu ili kuepuka kuvunja sheria.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG