Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Oktoba 01, 2023 Local time: 15:34

Museveni akabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wengine 10 wakiwemo majenerai wenzake 2


Rais Yoweri Museveni

Kampeni kuelekea uchaguzi mkuu nchini Uganda zimeanza, baada ya tume ya uchaguzi kumaliza zoezi la kuwasajili wagombea wa urais, ubunge, na viongozi wa serikali za mitaa.

Rais wa sasa Yoweri Museveni anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wengine 10, akiwemo mwanamuziki Robert Kyagulanyo maarufu kama Bobi Wine, na majenerani wengine wawili ambao walikuwa marafiki wa karibu wa Museveni kabla ya kukosana.

Majenerali hao ni aliyekuwa waziri wa usalama Henry Tumukunde na aliyekuwa kamanda wa jeshi Mugisha Muntu.

Bobi Wine

Mwanamuziki ambaye sasa ni mgombea urais Robery Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, anayegombea urais kwa tiketi ya chama cha NUP, amefanya kampeni kubwa mjini Arua kaskazini mwa Uganda na kuvutia umati mkubwa wa watu hasa vijana.

Japo kampeni yake ilikuwa imepanga kukutana na idadi ndogo ya watu katika uwanja wa michezo mjini humo, umati mkubwa wa watu ulijitokeza barabarani na kusitisha shughuli mjini humo.

Mara ya mwishi Bobi Wine kufanya kampeni mjini Arua, ilikuwa katika uchaguzi mdogo mwaka 2018 ambapo ulimalizikakwa machafuko, kifo cha dereva wake na gari la rais Yoweri Museveni kuripotiwa kupigwa mawe.

Kyagulanyi mwenye umri wa miaka 37, ametoa wito kwa polisi kukoma kuhangaisha wafuasi wake, akisema kwamba kila mtu anastahili kuishi kwa kuheshimu mwingine na kwamba rai ana polisi ni mandugu, majirani na wate wanapitia changamoto zinazofanana.

“Tunapigwa na kunyanyaswa na polisi kila mara. Polisi ni ndugu zetu. Ni dada zetu. Ni jamaa wetu. Tuna ukoo nao lakini wanaedelea kutupiga kila mara. Ni vyema wajue kwamba hii nchi ni yetu sote na hatutachoka kudai haki hadi pale kila mtu atakapohisi amekombolewa.” amesema Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Museveni apiga kambi Lira

Rais Yoweri Museveni ambaye aliingia madarakani Bobi Wine akiwa na umri wa miaka 4, amefanya kampeni yake katika wilaya ya Lira kaskazini mwa Uganda.

Wilaya ya Lira inapakana na Arua ambapo amekuwa Bobi Wine.

siku moja baada ya kuzindua kampeni yake ya kutafuta mhula wa sita madarakani.

Uzinduzi wa kampeni ulifanyika katika wilaya ya Luweero.

Museveni amesema kwamba hataki kukutana na kundi kubwa la wafuasi wake jinsi ambavyo imekuwa katika kampeni zilizopita, kutokana na janga la virusi vya Corona.

Kampeni yake itakuwa ya kukutana na makundi ya watu wachache kutoka sehemu tofauti katika kila wilaya.

Akiwa mjini Lira, Museveni amesema kwamba mafuta ambayo yanatarajiwa kuanza kuchimbwa hivi karibuni, ni hatua nzuri sana itakayoimarisha uchumi wa mji huo na Uganda kwa jumla.

“Imetimia miaka 14 tangu tulipogundua kwamba tuna utajiri wa mafuta lakini kampuni za kuchimba mafuta zimekuwa zikituchelewesha kupata utajiri huo. Hatimaye tumekubaliana nao na sasa tutaanza kuchimba.” Amesema Museveni katika mkutano na wafuasi wa chama chake cha National resistance Movement NRM.

Ujumbe muhimu wa Museveni kwa wapiga kura ni kwamba anagombea mhula wa sita madarakani ili kulinda hali ya baadaye ya raia wote wa Uganda.

Gen. Mugisha Muntu, Gen. Tumukunde na Nobert Mao

Aliyekuwa kiongozi wa chama cha Forum for Democratic change, ambaye sasa ni kiongozi wa chama cha Alliance for National Transformation Maj gen Mugisha Muntu, amezindua kampeni yake jijini Kampala, akisisitiza kwamba jiji hilo lina changamoto nyingi ikiwemo mfumo mbovu wa usafiri licha ya kuwa kitovu cha uchumi wa Uganda.

“Kampala ni moyo wa nchi yetu lakini jiji hili limejaa changamoto chungu nzima ambazo zinaathiri kwa kiasi kikubwa sehemu nyingine za nchi. Hii inatokana na mipangilio mibovu ambayo imeathiri pia shughuli za biashara. Haya ni matatizo ambayo tutatatua tutakapoingia madarakani mwaka ujao 2021.” Amesema Mugisha Muntu.

Aliyekuwa waziri wa usalama Generali Henry Tukunde amefanya kampeni yake magharibi mwa Uganda katika wilaya za Rubanda, Rukiga na Kabale akiwahimiza wafuasi wake kumchagua kwa ahadi ya kile anataja kama “Uganda mpya.”

Tumukunde alifutwa kazi na rais Yoweri Museveni mwaka 2018 baada ya kutofautiana hadharani na aliyekuwa mkuu wa polisi Generani Kale Kayihura.

Amekamatwa na kufikishwa katika mahakama ya kijeshi, akidaiwa kumiliki sare na silaha za kijeshi.

Kiongozi wa chama cha Democratic – DP, Nobert Mao, anatarajiwa kuzindua kampeni yake Jumatano.

Kukosekana kwa Besigye katika kinyang’anyiro cha urais

Mgombea wa urais mara nne bila mafanikio Dkt Kiiza Besigye hayupo kwenye orodha ya wagombea mwaka huu baada ya kusema kwamba kuendelea kugombea nafasi hiyo dhidi ya rais Yoweri Museveni ni kupoteza muda.

Besigye amesema kwamba ana mpango mbadala wa kumuondoa madarakani Yoweri Museveni, japo hajasema wazi ni mpango gani na amesema kwamba atawafanyia kampeni wagombea ambao wanaunga mkono mpango wake.

Wagombea wa urais Uganda mwaka 2021

Wagombea wa urais ni 11. Wanaume 10 na mwanamke mmoja.

Orodha ya wagombea urais nikama ifuatayo

 1. Yoweri Kaguta Museveni
 2. Henry Tumukunde
 3. Kabuleta Joseph Kiiza
 4. Kalembe Nancy Linda
 5. Robert Kyagulanyi Sentamu
 6. Nobert Mao
 7. Patrick Amuriat Oboi
 8. Mwesigye Fred
 9. Katumba John.
 10. Mayambala Willy.
 11. Mugisha Gregory Muntu

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG