Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Februari 05, 2023 Local time: 16:48

Museveni: Mipaka ya Uganda itaendelea kufungwa kwa siku 21 zaidi


Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Mipaka ya Uganda itaendelea kufungwa kwa siku 21 zaidi, huku watu wakitakiwa kutotoka nje ya nyumba zao kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.

Hii ni baada ya rais Yoweri Museveni kuongeza mda wa amri karibu 36 alizotoa katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya Corona nchini humo kwa wiki tatu zaidi kuanzia leo jumanne.

Kulingana na Museveni, hatua yake ya kuongeza mda wa kusitisha shughuli za kawaida nchini humo, “itasaidia kushinda nguvu virusi vya Corona au kutoa mda wa kutosha kwa nchi kujitayarisha vizuri kukabiliana na virusi hivyo.”

Miongoni mwa hatua alizochukua rais huyo kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona ni kupiga marufuku usafiri wa magari, kufunga biashara ambazo sio muhimu isipokuwa uuzaji na ununuzi wa chakula na dawa.

Museveni amesema hatua alizochukua zimesaidia sana kukabiliana na maambukizi, na haziwezi kulegezwa kwa sasa hadi virusi hivyo vitakaposhindwa nguvu kabisa.

“Tusiwe kama mama aliyejifungua mtoto baada ya kufikisha miezi 8. Tusubiri hadi miezi 9. Tusikose Subira. Tusubiri kwa siku 21 zaidi,” alisema Museveni.

Wakati huo huo, Museveni ametangaza mipango ya kuwarudisha Uganda raia wa nchi hiyo ambao wamekwama nchi za nje kutokana na janga la Corona.

Amesema amemwelekeza waziri mkuu Dk. Ruhakana Rugunda na waziri wa mambo ya nje Sam Kutesa, kusimamia mpango wa kuwarejesha nyumbani raia wa Uganda waliokwama nje ya nchi.

Hii ni baada ya baadhi ya raia wa Uganda kupitia mitandao ya kijamii kusema wameishiwa na pesa kununua chakula katika nchi ambazo wamekwama.

“Nitazungumza na waziri wa mambo ya nje kujua mipango iliyopo kuwafikia raia wa Uganda waliokwama nje ya nchi na kuhakikisha tunawarudisha nyumbani. Hili ni jambo rahisi. Tutawasafirisha halafu tuwaweke karantini kwa mda. Hili linawezekana kabisa bila kuhatarisha Maisha ya wengine,” alisema Museveni katika hotuba kwa taifa Jumanne.

Mwito wa kuwarejesha nyumbani raia wa Uganda umetolewa wakati kuna ripoti za waafrika kudhulumiwa nchini China, kuhusiana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Tukio hilo limekashifiwa kote duniani, mataifa ya Afrika yakiandikia China kutaka likomeshwe mara moja.

Museveni hata hivyo amesema huenda ikawa vigumu kutekeleza agizo la kuwaondoa raia wake katika nchi ambazo zimefunga mipaka yake kama Marekani.

“kwa mfano, ni vigumu kuwaondoa raia wa Uganda walio Marekani kwa sababu wanaishi sehemu mbalimbali na usafiri nchini humo unazuiliwa. Hatuwezi kutuma ndege kutafuta kila mtu mahali alipo,” ameeleza Museveni.

Watu 54 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona nchini Uganda kufikia Jumanne.

Idadi kubwa ya walioambukizwa ni wale walioingia Uganda kutoka nchi za nje hasa Dubai.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG