Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Oktoba 07, 2024 Local time: 10:34

Mtoto wa Afrika anapaswa kulindwa


Wakati Afrika ikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, nchini Tanzania migogoro ya familia na kutengana kwa wazazi vimeendelea kuwa sababu kubwa inayopelekea watoto wengi kuishi katika mazingira magumu, kukatisha masomo, na kujiingiza katika utumikishwaji wa kazi wakiwa na umri mdogo.

Huku wazazi wanatakiwa kuendelea kutoa malezi bora kwa watoto wao hata baada ya kutengana.

Miriam Enock, mtoto kutoka Bukoba, ni mfano hai wa athari hizo ambaye kwa sasa anaishi katika kituo cha kulelea watoto huko Shinyanga baada ya kupitia changamoto nyingi kutokana na kutengana kwa wazazi wake.

Baada ya wazazi wake kutengana, yeye na wadogo zake walilazimika kuondoka na kwenda kuishi na mama yao mkoani Bukoba. Huko walikumbana na ugumu wa maisha uliowalazimu Miriam na mama yake kutafuta shughuli ndogondogo za kujikimu.

"Mara nyingi, ilibidi nifanye kazi au kutafuta kibarua kama ni cha kulima, na ikiwa nikipata hela ndipo tungeweza kula nyumbani," alisema Miriam.

Na kuongeza kuwa "Mama alikuwa akitafuta kazi upande mmoja, mimi upande mwingine, na mdogo wangu pia. Lengo lilikuwa kupata hela ya kula ili tuweze kuwalisha wadogo zetu."

Miriam anaongeza kuwa kutokana na hali duni ya maisha, ilimlazimu kuanza kufanya kazi za ndani, jambo lililompelekea kukatisha masomo yake pamoja na wadogo zake na kutokana na umri wake mdogo, alijikuta akipitia vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika familia ambazo alikuwa akifanyia kazi, na hivyo kukimbilia katika kituo cha kulelea watoto.

Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE lililopo Shinyanga, John Myola, ambalo linajishughulisha na uokoaji wa watoto wa kike waliopitia vitendo mbalimbali vya ukatili, amewataka wazazi kuendeleza watoto wao kielimu hata baada ya kutengana ili kuwasaidia watoto hao kufikia ndoto zao.

"Mimi niombe tu hasa wanaume kwamba, wanapokuwa wametengana, wakumbuke kwamba wale watoto ni wa kwao. Waendelee kuwaendeleza na wasiwaache. Waendeleze watoto wao kielimu. Naamini kwamba urithi bora kwa mtoto ni elimu, kwa hiyo ni muhimu kuendelea kuwaendeleza watoto wao," alisema Myola.

Myola anaongezea kuwa serikali inapaswa kujenga vituo vingi zaidi kwaajili ya kusaidia watoto mbalimbali ambao wanapitia changamoto pamoja na kupunguza masharti ya watoto kuingia katika vituo hivyo kwakuwa masharti hayo yamekuwa yakikwamisha jitihada za kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

“Serikali ina kituo Dodoma ila imekuwa ngumu watoto kupata nafasi kuingia katika kituo hicho, yaani wakati mwingine serikali yetu imekuwa inafanya vitendo vibaya sana inatengeneza vituo vya kulelea watoto lakini wanaweka masharti utadhani mtu anaenda mbinguni, kwahiyo hivi vitu vinakuwa sio vizuri sana kwa watoto” amesema Myola

Hata hivyo, George Bwile, Mkurugenzi wa Taasisi ya TAYOTA iliyopo jijini Tanga, amesema serikali inapaswa kuangalia namna gani inaweza kuziwezesha taasisi zinazosaidia watoto ambao wanapitia changamoto mbalimbali, ikiwemo kukosa malezi kutokana na familia kutengana, ili kuziwezesha kupata fedha za kuhudumia watoto hao.

"Wito wangu kwa serikali ni kuweza kuangalia jinsi gani kwa kupitia wizara ya maendeleo ya jamii na jinsia kuweza kuwawezesha hasa kifedha nyumba salama katika uendeshaji wake, hasa zile ambazo haziendeshwi na serikali. Kuna wadau wengi ambao pia wameanzisha hizi nyumba salama wao binafsi tu kwa mapenzi yao kwa watoto lakini wanakosa ufadhili," alisema Bwile.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yamebeba kauli mbiu isemayo “Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi,” ikisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ambayo ni kamilifu na inayomwandaa mtoto kwa maisha ya baadaye kwa kuwapatia maarifa muhimu, maadili mema, na stadi za kazi zinazohitajika.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG