Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 06, 2022 Local time: 04:04

Kenya: Mtangazaji mkongwe Mohamed Juma Njuguna aaga dunia


Mtangazaji mkongwe wa Kenya, Mohamed Juma Njuguna.

Mtangazaji mkongwe na aliyekuwa na umaarufu mkubwa nchini Kenya, Mohamed Juma Njugua, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Kwa mujibu wa familia, Njuguna alikuwa amelazwa hospitalini kwa wiki tatu kabla ya kifo chake.

Njuguna, ambaye alifanya kazi hiyo kwenye vituo mbalimbali vya televisheni na redio kwa takriban miongo minne, aliaga dunia Jumamosi katika hospitali moja mjini Nairobi.

Alikuwa mmoja wa watangazaji walioenziwa tangu miaka ya 70, kama magwiji katika taaluma hiyo.

Kabla ya kuugua, mtangazaji huyo alikuwa mzalishaji wa vipindi katika kituo cha Radio Citizen kinachomilikiwa na kampuni ya Royal Media Services.

Mwanahabari huyo atakumbukwa kwa umahiri wake wa utangazaji kwa lugha ya Kiswahili, hususan matangazo ya moja kwa moja ya mechi za kandanda.

Njuguna alipata tuzo la rais wa Kenya iitwayo Head of State Commendation (HSC) mnamo mwaka wa 2010 kwa mchango wake katika kukuza sekta ya mawasiliano nchini humo.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, Njuguna alizikwa Jumamosi alasiri katika makaburi ya Kiislamu ya Kariokor mjini Nairobi.

Mtangazaji huyo amemwacha mjane na watoto kadhaa.

Mungu na ailaze roho yake pema peponi.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG