Huduma za mtando wa internet zimekuwa hafifu katika baadhi ya maeneo Afrika Mashariki kwa karibu siku nne sasa kutokana na kuharibika nyaya zinazopita chini ya bahari ambazo zinawezesha huduma hiyo kwa haraka.
Kampuni ya Seacom inayomiliki nyaya hizo imesema bado inachunguza nini hasa kilichosababisha tatizo hilo, lakini inadhaniwa tatizo hilo liko katika mwambao wa Kenya.
Mtandao huo uliomalizika kujengwa mwaka 2009 unaunganisha nchi za Afrika kusini, Tanzania, Kenya, Uganda na Msumbiji kuelekea Ulaya na Asia.
Seacom ilisema imeanza matengenezo ya dharura ambayo yanaweza kuchukua siku nane. Tatizo hili la ghafla limeathiri mawasiliano kwenda India na Ulaya. Kwa mujibu wa taarifa hiyo wateja ndani ya Afrika hawajaathirika sana na tatizo hilo.
Kampuni hiyo ilisema ilikuwa ikifanya kazi tangu tatizo hilo liliporipotiwa Julai 5 mwaka huu kutafuta njia nyingine za kuwezesha mawasiliano ya internet, ikiwemo nyaya mbadala.