Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 03:06

Mtaala mpya wa elimu ya Kenya kuboreshwa, sio kufutiliwa mbali


Wanafunzi wa shule ya msingi ya Toi, jijini Nairobi, Kenya wakiwa darasani. September 6, 2011
Wanafunzi wa shule ya msingi ya Toi, jijini Nairobi, Kenya wakiwa darasani. September 6, 2011

Rais wa Kenya Dr. William Ruto anatarajiwa kuunda jopokazi la kutathmini utekelezwaji wa Mtaala wa elimu wa Umilisi na Kuzingatia Umahiri maarufu kama CBC ili kuuboresha lakini sio kuufutilia mbali, naibu wake Rigathi Gachagua ameeleza na kuonesha kuondokea matamshi ya awali ya kufuta mtaala huo.

Naibu rais wa Kenya amesema kuwa jopo kazi hilo litakaloundwa litaangazia maeneo yanayotia wasiwasi katika mtaala huo kwa kushauriana na washikadau husika wakiwemo wazazi kupitia ushirikishwaji wa umma ili kuimarisha maendeleo ya jumla ya wanafunzi.

Wataalamu na washikadau wa elimu wanasema kuwa uhakiki huo unahitaji kufanywa kwa nia iliyo wazi.

Matamshi ya Gachagua yanatajwa kuwa afueni kwa baadhi ya wazazi, walimu na wanafunzi pamoja na washikadau wengine waliokuwa wamewekeza zaidi katika utekelezaji na ufanisi wa mtaala huo wa elimu wa Umilisi na unaozingatia umahiri maarufu kama CBC.

Wataalam wa elimu wanataka mabadiliko katika mtaala

Wataalam wa elimu wanaeleza kuwa tathmini inayostahili kufanyikia mtaala huo inastahili kuwa na kusudi la kuondoa vizingiti na kuziba mianya iliyopo kuhusu mfumo huo, anavyoeleza Kombo Kikechi, mtaalam wa elimu nchini Kenya anayeleza kuwa jopo kazi linaloundwa sharti lizingatie maendeleo ya mwanafunzi na kurahihisha nyezo za mafunzo kutoka kwa walimu.

Tangu serikali ya Rais wa Kenya William Ruto itangaze pendekezo la kubuni jopo kazi la kuchunguza utekelezaji wa mtaala huo, pamekuwa na wasiwasi kuwa huenda ukafutiliwa mbali, yalivyokuwa maoni ya baadhi ya wandani wa Bw Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi mapema mwaka huu, kuashiria kuwa mtaala huo ni mzigo mzito kwa taifa.

Gachagua, kwa sasa ameondoa wasiwasi huo na kuwahakikishia wazazi kuwa nia ya serikali ni kuuboresha mtaala huo wala si kuufutilia mbali.

Wazazi kushirikishwa katika ushauriano kuhusu mtaala wa elimu

Gachagua anaeleza kuwa jopo kazi hilo litakaloundwa litaangazia maeneo yanayotia wasiwasi katika mtaala huo kwa kushauriana na washikadau husika wakiwemo wazazi kupitia ushirikishwaji wa umma ili kuimarisha maendeleo ya jumla ya wanafunzi.

Mtaala huo wa Umilisi na Kuzingatia Umahiri wa mwanafunzi umekuwa ukitajwa kuwa mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini Kenya kwani unaondoa mitihani ya kitaifa na kuwezesha mwendelezo wa tathmini kuangalia uwezo wa wanafunzi.

Mtaala huo wa 2-6-3-3-3 unatekelezwa awamu kwa awamu na unahimiza uwezo wa mwanafunzi katika taaluma na nyanja mbalimbali.

CBC unavyojulikana nchini Kenya, unaomwezesha mwanafunzi kusoma miaka miwili katika shule za chekechea, miaka sita katika shule za msingi, miaka mingine sita katika shule za upili na miaka mitatu katika chuo kikuu, unatajwa nchini Kenya kuwa mabadiliko muhimu yasiowafanya wanafunzi kuwa watumwa wa mitihani bali unahimiza na kukuza uwezo wao kupitia talanta na ubunifu katika nyanja mbalimbali.

Mtaala wa elimu wa 8-4-4 umekosolewa kwa kukosa kusuluhisha changamoto za sasa maishani

Tangu mwaka wa 1985, Kenya imekuwa na mifumo mitatu ya elimu, na mfumo ambao umekuwa ukitumika wa 8-4-4 ambako mwanafunzi anasoma miaka minane katika shule ya msingi, miaka minne katika shule ya upili na miaka mingine minne katika vyuo chuo kikuu, unatajwa kusisitiza na kuhimiza sana mitihani.

Mtaala wa CBC ulivyo, unapendekeza kuondolewa kwa mitihani ya kitaifa na badala yake kuwapo na mwendelezo wa tathmini kutathmini uwezo wa wanafunzi, kulingana na ubunifu na talanta yake, hapa walimu, wazazi na jamii pana zikitajwa kuwa nguzo kuu katika ufanikishaji wake.

Wanafunzi wanafanyiwa tathmini kwa asilimia 20% katika gredi ya nne, tano, sita na kwa asilimia 40% mwishoni mwa mafunzo ya gredi ya sita ili kupima uwezo na nguvu za kuingia katika hatua nyingine, ikiwa ni sehemu ya alama za mwisho kwa asilimia 100% mwishoni mwa shule ya msingi.

Katika miaka mitatu ya kidato cha chini yaani wanafunzi wanaosoma shule ya upili kwa miaka mitatu ya kwanza mfululizo watakuwa na masomo 12 na mengine ya ziada yakiwa ni ya kujiteulia kulingana na uwezo na talanta ya mwanafunzi husika, lengo likiwa ni kuendeleza taaluma aliyoteua mwanafunzi huyo.

Na miaka mitatu mingine katika shule ya upili, wanafunzi watakuwa na majawabu matatu ya masomo; kwanza; masomo ya uhandisi, sayansi na kiufundi, pili masomo ya kijamii, na tatu spoti na Sanaa; kila kitengo kikiwa na wanafunzi kivyake kama ilivyo katika vyuo vikuu.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG