Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 17, 2025 Local time: 18:47

Msumbiji: Chanjo dhidi ya kipindupindu kutolewa kwa kila mtu katika sehemu zilizopigwa na kimbunga


Afisa wa serikali akipokea chanjo dhidi ya kipindupindu
Afisa wa serikali akipokea chanjo dhidi ya kipindupindu

Maafisa wa afya nchini Msumbiji wanajitayarisha kuanza kutoa chanjo dhidi ya kipindupindu katika mji wa Quelimane, ambao umeshuhudia uharibifu mkubwa kutokana na kimbunga Freddy kilichopiga mapema mwezi uliopita.

Mkurugenzi wa afya katika jimbo la Zambezia, Blayton Caetano ameiambia radio ya serikali ya Msumbiji kwamba zoezi la kutoa chanjo dhidi ya kipindupindu litachukua muda wa wiki mbili.

Shughuli hiyo inalenga kupunguza maambukizi ya kipindupindu ambapo idadi yake ilikuwa juu mno baada ya kimbunga cha kihistoria.

Uharibifu mkubwa ulitokea Quelimane kutokana na kimbunga Freddy kilichoua watu 19 na kupelekea watu 50,000 kupoteza Makazi.

Caetano amesema kwamba kila mtu katika mji huo atapatiwa chanjo dhidi ya kipindu pindu ili kuzuia maambukizi.

"Tupo tayari kuanza kutoa chanjo katika muda was aa 24 au 48 zijazo. Tutauangazia zaidi mji wa Quelimane. Lengo kubwa ni kwamba wakaazi wote wa Quelimane wanapata chanjo hiyo. Tunataka kuhakikisha kwamba maambukizi ya kipindupindu yanapungua kabisa katika muda wa wiki mbili."

Shirika la kuwahudumia Watoto la umoja wa mataifa UNICEF, limesema katika taarifa kwa vyombo vya habari hivi karibuni kwamba karibu watu 10,000 wameambukizwa kipindupindu kote nchini Msumbiji, ikiwa ni mara tatu ya ya maambukizi ikilinganiswa na mwezi Februari.

Msumbiji imesema Jumanne kwamba imepokea dozi milioni 1.7 za chanjo dhidi ya kipindupindu. Chanjo hiyo imetolewa na UNICEF.

Wizara ya afya imesema kwamba chanjo hiyo itatolewa kwa wakaazi wa Quelimane katika jimbo la Zambezia, Chimoio katika jimbo la Manica, na Beira pamoja na Marromeu katika jimbo la Sofala.

Mafuriko na uharibifu kwenye mfumo wa maji safi, uliosababishwa na kimbunga Freddy, umepelekea kuongezeka kwa maambukizi ya kipindupindu katika mji wa Quelimane.

Maelfu ya watu katika mji wa Quelimane wamekuwa wakisafiri mwendo mrefu wakitumia magari au kwa mguu wakitafuta maji safi ya kunywa na matumizi ya kawaida.

Idadi kubwa ya watu wanakunywa maji kutoka kwa vidimbwi.

Maafisa wa afya wameonya kwamba wanakaribia kukumbwa na uhaba mkubwa wa dawa kwa ajili ya kutibu maji na wametoa wito kwa watu kununua dawa hizo kwa maduka ya kibinafsi.

Wakati huo huo, Msumbiji inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika sehemu za kaskazini ambapo kuna makundi ya wapiganaji na takriban watu milioni 2 wanahitaji msaada katika sehemu hiyo.

XS
SM
MD
LG