Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 23, 2024 Local time: 16:58

Mwanachama wa Boko Haram afungwa miaka 15


Mshukiwa mwanamgambo wa Boko Haram akiwa na wasichana waliotekwa nyara
Mshukiwa mwanamgambo wa Boko Haram akiwa na wasichana waliotekwa nyara

Mtu mmoja kati ya watu waliohusika na utekaji nyara wa zaidi ya wanafunzi wasichana 200 kutoka katika mji wa Chibok kwenye jimbo la Borno huko Nigeria mwaka 2014 amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

Serikali ya Nigeria ilithibitisha hukumu iliyopitishwa dhidi ya Harun Yahya mwenye umri wa miaka 35 ikiwa ni hukumu ya kwanza kutolewa kuhusika na utekaji nyara huo wa watu wengi uliozusha hasira kote duniani na kuanzishwa kampeni ya kimataifa ya “Bring back Our Girls” ya kutaka wasichana hao kuachiliwa huru. Jumla ya wanafunzi 276 walitekwa katika shule ya serikali ya wasichana kutoka kwenye bweni lao usiku wa April 14 mwaka 2014.

Wanafunzi 57 waliweza kukimbia mara tukio hilo lilipotokea na wengine 107 wameweza kukimbia au wamepatikana au kuachiliwa kuanzia mwaka 2016 baada ya serikali kuanza mazungumzo na wanamgambo hao wenye itikadi kali wa Boko Haram. Kuna wasichana 112 ambao hawajapatikana bado. Kuna watu 1,669 wanaoshikiliwa kuhusika na shambulio hilo ambao wanasubiri kufunguliwa mashtaka au kesi zao kusikilizwa.

Msemaji wa wizara ya sheria Salihu Isah alisema Yahya alikiri kuhusika alipofika mbele ya mahakama maalum inayosikiliza kesi ya mamia ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni wanachama wa Boko Haram.

XS
SM
MD
LG