Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 22, 2024 Local time: 19:29

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sarah Sanders kujiuzulu


Msemaji wa White House Sarah Huckabee Sanders (Katikati)
Msemaji wa White House Sarah Huckabee Sanders (Katikati)

Sarah Huckabee Sanders, msemaji wa Ikulu ya Marekani, ataondoka kwenye wadhifa huo mwishoni mwa mwezi Juni.

Rais Donald Trump alitangaza hayo Alhamisi alasiri na kuelezea matumaini yake kwamba Sanders atawania kiti cha gavana wa jimbo la Arkansas "kwa sababu anaiweza vizuri sana kazi hiyo."

Trump alisema Sanders amehudumu kwa miaka mitatu unusu, ikiwa ni pamoja na wakati alipokuwa kwenye kampeni yake ya 2016.

"Ni mtu maalum mwenye vipawa vya kipekee na aliyefanya kazi ya ajabu. Ninamshukuru na kumpongeza sana," aliandika Trump.

Akizungumza muda mfupi baada ya Trump kuandika ujumbe huo, Sanders alisema daima atajivunia kazi aliyoifanaya kama msemaji wa Ikulu.

"Nimependa kila dakika ya kazi yangu...nyakati nzuri na hata zilizokuwa ngumu," alisema.

Sanders, mwenye umri wa miaka 36 na bintiye aliyekuwa gavana wa 44 wa jimbo la Arkansas, Mike Huckabee, ametajwa na wachambuzi kama mmoja wa watetezi wakuu wa sera za Rais Trump ambaye mara kwa mara, alijibizana vikali na baadhi ya waandishi wa habari hususan wakati wa maswali na majibu katika ikulu.

Msemaji huyo wa Ilkulu alichukua wadhifa huo mwezi Julai mwaka 2017 baada ya aliyemtangulia, Sean Spicer, kujiuzulu. Amekuwa msemaji wa 28 wa White House tangu nafasi hiyo kubuniwa.

Sanders anaondoka wakati ambapo baadhi ya mashirika ya habari ya Marekani yamekuwa yakilalamika kwamba kwa zaidi ya siku 90, hajakuwa na kikao na waandishi kwenye ikulu kama ilivyokuwa desturi.

Haikufahamika mara moja ni nani atakayeteuliwa na Rais Trump kuchukua nafasi ya Sanders.

XS
SM
MD
LG