Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 18, 2024 Local time: 23:47

Msamaha wa Rais : Ingabire, Mihigo wampongeza Kagame


Kizito Mihigo akitoka gerezani nchini Rwanda
Kizito Mihigo akitoka gerezani nchini Rwanda

Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda Victoire Ingabire aliyeachiwa huru, kwa msamaha wa Rais Paul Kagame, amesema kuachiwa huko ni ishara kuwa uwanja wa siasa unaboreshwa zaidi.

Mwanasiasa huyo aliyekuwa amehukumiwa miaka 15 jela kwa kosa la uhaini ameyasema hayo mara baada ya kuachiwa huru.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa Ingabire, wa chama cha upinzani cha FDU Inkingi na ambacho hakijasajiliwa nchini Rwanda, ni miongoni mwa wafungwa zaidi ya 2,000 walioachiwa huru mwishoni Jumamosi kwa msamaha wa Rais Paul Kagame.

Kauli ya Ingabire baada ya kutoka jela

Ingabire amesema : "Nimekuwa nikifuatilia nikiwa gerezani hali ya mambo inavyo endelea nchini, kuna mafanikio mengi yaliyofikiwa, na ninadhani tunaweza kupiga hatua zaidi tukishirikiana pamoja kwa sababu kuna mengi ya kufanya. Hii ndiyo njia nzuri ya kujenga nchi yetu kwa kuheshimu mawazo ya wale tunaohisi nii wapinzani, nampongeza Rais ambaye ameamua kunipa msamaha na kutoka nje ya gereza."

Ingabire amekuwa gerezani tangu mwaka 2013, baada ya Mahakama ya Rufaa kumkuta na hatia ya uhaini na kumpa kifungo cha miaka kumi na mitano jela.

Alikamatwa baada ya kurejea nchini kutoka Uholanzi alipokuwa uhamishoni kwa miaka 16 na kugombea kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Wakati huo huo mwanamuziki wa nyimbo za dini Kizito Mihigo ambaye alikuwa amehukumiwa miaka 10 jela kwa kosa la kuhatarisha usalama wa nchi, naye ameachiwa huru kwa msamaha wa Rais.

Wawili hao wamekuwa wakitajwa na vyombo vya habari vya kimagharibi kama wapinzani wa serikali kwa kushirikiana na mahasimu wa serikali walioko uhamishoni.

Kauli ya Kizito baada ya kuachiwa

Kizito ameieleza VOA : "Mimi nampongeza Rais Paul Kagame kwa uamuzi wake wa kuniachia huru, huu ni uamuzi unaobainisha uwezo wake wa kuamua mambo, huu ni uamuzi wenye faida kwangu, lakini pia ni uamuzi ambao utalisaidia taifa kwa sababu utaleta umoja na maridhiano miongoni mwetu sisi kama raia wa Rwanda."

Kadhalika msanii huyu wa nyimbo za dini lakini zilizokuwa na mwelekeo ya umoja na maridhiano miongoni mwa wananchi amesema ataendelea na mkakati wake kutunga nyimbo zenye kuunganisha jamii ambayo yeye anaitaka kama inayohitaji maridhiano zaidi.

Kuachiwa huru kwa wawili hao sambamba na maelfu ya watu wengine umekuja siku moja baada ya baraza la mawaziri chini ya uongozi wa Rais Paul Kagame kutangaza uamuzi huo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Sylvanus Karemera, Rwanda.

XS
SM
MD
LG