Mlipuko umeshambulia gari la kijeshi kwenye msafara wa kijeshi mashariki mwa Kenya ljumaa na kujeruhi vibaya maafisa watatu wa kijeshi.
Mlipuko huo umetokea nje kidogo ya mji wa Garrisa katika barabara inayoelekea kwenye kambi kubwa ya wakimbizi ya Dadaab na kuelekea kwenye mpaka wa Somalia kiasi cha kilometa 150.
Maafisa wanachunguza kama ni bomu la kutegwa ardhini au ni bomu lililosababisha mlipuko huo au nani anayehusika na mlipuko huo.
Mashambulizi kwenye ardhi ya Kenya yameongezeka tangu majeshi yake yalipoingia Somalia wiki mbili zilizopita kuwasaka wanamgambo wa al-Shabab.
Wakati huo huo, mahakama moja ya Kenya ilimhukumu mtu mmoja kifungo cha maisha jela kwa moja ya mashambulizi mawili ya bomu ambayo yalitokea huko Nairobi Jumatatu.
Mapema wiki hii Elgiva Bwire Oliacha alikiri kuwa mwanachama wa Alshabab na kushiriki kwenye shambulizi katika kituo cha basi liliouwa mtu mmoja na kujeruhi wengine 20.