Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 26, 2024 Local time: 12:03

Misaada yazuiliwa kuingia Tigray Ethiopia


Watu waliokoseshwa makao kutokana na vita vya Tigray wakiwa wanasubiri kupewa chakula cha msaada katika mji wa Mekele, Ethiopia May 9, 2021.
Watu waliokoseshwa makao kutokana na vita vya Tigray wakiwa wanasubiri kupewa chakula cha msaada katika mji wa Mekele, Ethiopia May 9, 2021.

Shirikisho la kimataifa la Msalaba Mwekundu, limesema kwamba Juhudi za kufikisha misaada ya dawa katika eneo la Tigray, lililokumbwa na vita, zimeshindikana.

Hii ni licha ya sitisho la mapigano kati ya serikali na majeshi ya Tigray, ya kuruhusu misaada kuingia sehemu hiyo.

Shirikisho la Msalaba Mwekundu ICRC, limeruhusiwa kufikisha misaada katika eneo la Tigray tangu Januari mwaka huu, baada ya miezi ya kuzuiliwa, lakini linasema kwamba hakuna gari la shirikisho hilo ambalo limeruhusiwa kuingia sehemu hiyo kwa sababu za kiusalama.

Ndege 38 zilizokuwa zimebeba dawa zinazohitajika sana , ziliwasili Tigray zaidi ya miezi mitatu iliyopita.

Msemaji wa ICRC nchini Ethiopia Fatima Sator, amesema kwamba misaada iliyofikishwa sehemu hiyo haitoshi kabisa.

Mashirika ya misaada yamekuwa yakiishutumu serikali kwa kuzuia misaada kuwafikia watu wa Tigray, shutuma ambazo serikali ya Addis Ababa imekanusha.

Wakati sitisho la mapigano lilipotangazwa wiki iliyopita, kulikuwa na matumaini kwamba misaada ya kibinadamu ingewafikia mamilioni ya watu kwa haraka, katika eneo la Tigray.

Lakini serikali na wapiganaji wa Tigray wanaendelea kushutumiana na hakuna makubwa yaliyobadilika kuhusiana na misaada kuwafikia watu.

Shirikisho la Msalaba Mwekundu limesema kwamba hatua ya kuruhusu malori yenye misaada kuingia eneo hilo itakuwa ya muhimu sana.

XS
SM
MD
LG