Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Juni 23, 2024 Local time: 07:57

Wanasayansi wagundua njia ya kiteknolojia kupunguza hewa chafu


Watafiti wa kisayansi katika eneo la Iceland wamesema kuwa huenda wamegundua teknolojia mpya ambayo inaweza kupunguza hewa inayochafua mazingira, kwa kunasa hewa ya sumu ya carbon dioxide na kuigeuza kuwa mawe.

Jarida la 'American Scientist' limeripoti kuwa wanasayansi huko Iceland waliweza kuyeyusha hewa ndani ya maji na kupuliza mchanganyiko wake ardhini, ambako ilichanganyika na madini ya volcano, na kuunda mawe yanayofanana na chokaa.

Mradi huo uliopewa jina la 'CarbFix' una uwezo wa kunasa hewa ya sumu kutoka angani, na kuipenyeza kupitia kwenye mabomba na maji hadi ardhini.

Wanasayansi wamesema kwamba teknolojia hiyo mpya, huenda ikasaidia kukabiliana na mabadiliko ya viwango vya joto duniani, na kuongeza kuwa ni rahisi kwa mfumo huo kufaulu kwa sababu mawe ya volcano yanayohitajika kugeuza gesi hiyo, yanapatikana kote duniani.

Ingawa utafiti huo ambao umeendelea kwa miaka miwili uligharimu kiasi kikubwa cha fedha, wanasayansi wanaamini teknolojia hiyo mpya itakuwa ya manufaa kwa dunia ambayo inaendelea na kutafuta mbinu za kupunguza hewa chafu, hasa itokayo na viwanda vikubwa vinavyotumia kemikali kutengeneza bidhaa zake.

Kufikia sasa, mradi huo umegharimu takriban dola milioni 10.

XS
SM
MD
LG