Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 03:37

Mpaka kati ya Kenya na Somalia umefunguliwa, Miraa kutoka Kenya kuingia soko la Somalia


Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akisherekea ushindi wake kama rais wa 10 wa Somalia, mjini Mogadishu June 9, 2022. PICHA: AFP
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akisherekea ushindi wake kama rais wa 10 wa Somalia, mjini Mogadishu June 9, 2022. PICHA: AFP

Serikali ya Somalia imefungua tena soko lake kwa miraa kutoka Kenya baada ya kupiga marufuku uagizaji wa miraa kutoka nchi hiyo jirani, miaka 2 iliyopita.

Mpaka wa ardhi kati ya nchi hizo mbili utafunguliwa baada ya miaka 10 tangu ulipofungwa rasmi.

Safari za shirika la ndege la Kenya airways zimeruhusiwa kuanza safari za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Mogadishu.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mkutano kati ya rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, katika ikulu ya rais ya Nairobi, Kenya.

Kukarabati uhusiano wa kidiplomasia ulioharibika

Hatua hiyo ni mafanikio makubwa ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ambao umekuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni na kusababisha hasara ya kifedha kwa nchi zote mbili.

Kulingana na muungano wa wakulima wa miraa nchini Kenya, nchi hiyo imekuwa ikipoteza shilingi milioni 6(Dola 50,000) kila siku tangu Somalia ilipopiga marufuku bidhaa hiyo kuingia nchini mwake mwezi March 19, 2020.

Ikiwa ziara yake ya Kwanza nchini Kenya tangu alipochaguliwa kuwa rais, Mohamud amesema kwamba yupo tayari “kukarabati uhusiano kati ya Somalia na Kenya kwa kuzingatia heshima baina ya nchi hizo mbili na kushirikiana katika kutatua changamoto zinazozikumba nchi hizo.”

Somalia itauza Samaki nchini Kenya.

Kenyatta na Mohamud wamekubaliana kuimarisha biashara na ukuaji wa uchumi kati ya Somalia na Kenya.

“Kuna mambo mengi yanayotuleta Pamoja kuliko yale yanayotutenganisha. Sote tunakabiliwa na changamoto za kiusalama na ukame. Tuna changamoto kubwa.” Amesema rais Mohamud.

Uhusiano mbaya kati ya Kenya na Somalia

Uhusiano kati ya Kenya na Somalia ulikuwa umedorora wakati wa utawala wa Farmajo.

Somalia ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na Kenya mnamo mwaka 2020 kutokana na shutuma za ‘Kenya kuonyesha dalili za kutambua Somaliland kuwa nchi kamili’ Uhuru Kenyatta alipofanya mkutano na rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi katika ikulu ya Nairobi, Desemba 2020.

Somaliland ilijitenga kutoka kwa Somalia, ina serikali na sarafu yake lakini Somalia imekataa kuitambua kama nchi huru.

Kufuatia mkutano wa Ijumaa, Kenya imelegeza msimamo wake kuhusu utoaji wa visa kwa raia wa Somalia wanaotaka kuingia Kenya. Wamiliki wa pasipoti za kawaida watakuwa wakituma maombi ya viza kupitia kwa internet na zitashughulikia ndani ya mda wa siku 10 za kufanya kazi.

Vita dhidi ya Ugaidi

Somalia na Kenya zimeahidi kuendelea na ushirikiano wa kupambana na ugaidi

Somalia imekuwa ikisumbuliwa kwa mda mrefu na kundi la kigaidi la Al-shabaab.

Wanajeshi wa Kenya KDF, wapo nchini Somalia chini ya jeshi la umoja wa Afrika Amisom, kupambana na wanamgambo hao wenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Mzozo wa umiliki wa sehemu ya bahari hindi

Mpaka kati ya Kenya na Somalia una urefu wa kilomita 700. Nchi hizo mbili zimekuwa zikizozana kuhusu umiliki wa sehemu ya bahari hindi.

Mnamo mwezi Oktoba mwaka 2021, mahakama ya umoja wa mataifa ya kusuluhisha migogoro ICJ, iliamua kwamba Somalia inamiliki kiasi cha kilomita 100,000 mraba kwenye mpaka unaozozaniwa.

Sehemu hiyo ya bahari hindi ina utajiri mkubwa wa Samaki na madini.

Somalia imekuwa ikiishutumu Kenya kwa kile imekuwa ikitaja kama “kuingilia mambo yake ya ndani” huku Kenya ikiishutumu Somalia kwa “kutumia visingizio kuhepa kuajibika na kusuluhisha matatizo yake ya ndani.”

Kulingana na hesabu ya serikali ya Kenya, asilimia 5 ya bidhaa zinazouzwa Afrika kutoka Kenya, zinaingia katika soko la Somalia, ikiwa ni bidhaa za thamani ya shilingi bilioni 13 (Zaidi ya dola milioni 110).

Bidhaa za Somalia zinazoingia Kenya zinajumulisha thamani ya shilingi milioni 106 (dola 905,000) kila mwaka.

Imetayarishwa na Hubbah Abdi, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG