Morocco imemuita balozi wake nchini Tunisia siku ya Ijumaa baada ya Rais wa Tunisia Kais Saied kumpokea mkuu wa vuguvugu la Polisario Front linalodai uhuru wa Sahara Magharibi, eneo ambalo Morocco inalichukulia kuwa ni la kwake.
Morocco ilisema uamuzi wa Tunisia kumwalika Brahim Ghali kwenye mkutano huo wa kilele wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ambao unafanyika mjini Tunis ni "kitendo kikubwa kisicho na kifani ambacho kinaumiza sana hisia za watu wa Morocco".
Tunisia ni mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika, unaojumuisha wakuu wa nchi kadhaa za Afrika.
Tunisia, katika kujibu uamuzi wa Morocco, ilitangaza kuwa inamwita balozi wake nyumbani Rabat kwa mashauriano.