Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 22:47

MONUSCO yapongeza hukumu iliyotolewa na mahakama dhidi ya Ntabo Ntaberi


Ntabo Ntaberi Sheka, kiongozi wa kundi la NDC huko Congo
Ntabo Ntaberi Sheka, kiongozi wa kundi la NDC huko Congo

Mkuu wa MONUSCO anaamini uamuzi uliotolewa na mahakama ya kijeshi huko Goma unathibitisha uamuzi wa mamlaka ya Kongo kuendelea kwa msaada wetu, mapigano ya kisheria dhidi ya wahalifu wote wa vita nchini DRC

Kiongozi wa zamani wa wanamgambo huko Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo-DRC, Ntabo Ntaberi Sheka amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa makosa ya uhalifu wa vita na ubakaji wa watu wengi, uamuzi uliosifiwa na Umoja wa Mataifa kama ni pigo dhidi ya kutoadhibiwa kwa makundi yenye silaha nchini humo.

Katika taarifa iliyochapishwa Jumatatu, mkuu wa MONUSCO, Leila Zerrougui alipokea hukumu ya kifungo cha maisha kwa uhalifu wa vita uliofanywa na Ntabo Ntaberi “Sheka” kiongozi wa kundi lenye silaha la Nduma Defense of Congo-NDC. Leila anaamini kuwa uamuzi uliotolewa na mahakama ya kijeshi huko Goma unathibitisha uamuzi wa mamlaka ya Kongo kuendelea kwa msaada wetu, mapigano ya kisheria dhidi ya wahalifu wote wa vita katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, zamani na sasa.

Ntabo Ntaberi Sheka, alikutwa na hatia ya mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono na kuandikisha wanajeshi watoto walio chini ya umri wa miaka 15 , mahakama ya jeshi ilitoa uamuzi mwishoni mwa kesi yake iliyoendeshwa kwa miaka miwili.

Sheka alianzisha kundi la wanamgambo la Nduma Defence of Congo-NDC, linalofanya harakati zake katika jimbo la Kivu kaskazini huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, mahala ambapo alidai kuwa anapambana na waasi wa kihutu wa FDLR kutoka Rwanda.

Ntabo Ntaberi Sheka
Ntabo Ntaberi Sheka

Hati ya kukamatwa kwake ilitolewa Januari mwaka 2011, baada ya mfululizo wa mashambulizi ambayo NDC na makundi mengine mawili yanashutumiwa kubaka watu takribani watu 400 katika vijiji 13, kati ya Julai 30 na Agosti 2 mwaka 2010.

Elsa Taquet, mshauri wa masuala ya sheria kwa program ya Maziwa Makuu ya kundi lisilo la kiserikali la TRIAL International, anasema mashariki mwa DRC haijawahi kushuhudia hukumu ya kiwango kama hicho.

“Kwa hali yeyote, tunashuhudia wakati wa kihistoria. Sheka amepatikana na hatia ya uhalifu wa vita, ni mtu ambaye hakika hakuna mtu yeyote aliyedhani wangewahi kumuona kizimbani, kwa hivyo hii ni hatua kubwa kusonga mbele katika upatikanaji haki”

NDC pia ilishutumiwa kuwapatia mafunzo angalau Watoto 154 katika safu zake za kijeshi.

Wanajeshi wake walilaumiwa kwa kuharibu takribani nyumba na biashara 1,000 pamoja na kuongoza kiasi cha watu 100 kuingia katika ajira za kulazimishwa. Taquet anasema hawajaridhishwa na hali Fulani ya uamuzi.

“Kuna mambo kadhaa ya uamuzi ambayo tumeyafurahia kiasi, kwa mfano kutambuliwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu kwa ubakaji huko Luvungi, lakini uhalisia au ukweli unabaki kuwa hivyo hivyo kwa ujumla, ni uamuzi mzuri sana uliotoa matumaini na ujumbe mzuri kwa waathiriwa kwamba sheria imetendeka”.

Lakini Kahindo Fatuma, msemaji anayewawakilisha waathirika, aliliambia shirika la Habari la AFP kwamba, “Tumefurahishwa na hukumu hii, ni ishara tosha kwa wababe wengine wa vita”, aliongeza kuwa waathirika watapata faraja kidogo.

Mmoja wa washtakiwa wenzake, pia alihukumiwa kifungo cha maisha jela hiyo Jumatatu, mwingine kifungo cha miaka 15 na wa mwisho aliachiliwa huru, kulingana na uamuzi wa mahakama ya jeshi ya uendeshaji ya Kivu kaskazini.

Dazeni ya makundi yenye silaha yanafanya harakati zake mashariki mwa DRC, eneo ambalo kuna ukosefu wa sheria lenye utajiri wa madini. Wamefanya vurugu kwa miongo kadhaa tangu kumalizika rasmi kwa vita vya mwaka 1998 mpaka 2003 ambapo mamilioni ya watu walipoteza maisha. NDC bado liko kwa jina jingine la NDC Renovate au NDC/R.

XS
SM
MD
LG