Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Juni 18, 2024 Local time: 11:38

Vijana wa Mombasa watumia maonyesho ya urembo kuhamasisha maadili mema


Maonyesho ya mitindo Mombasa
Maonyesho ya mitindo Mombasa

Maonyesho ya urembo baina ya wanamitindo mbalimbali yamekuwa maarufu katika mataifa ya Ulaya atangu miaka ya 1800.

Hata hivyo fani hii ya uanamitindo ilipoanza kuingia katika mataifa ya Afrika, sasa vijana wamechangamkia fani hiyo kwa kuandaa matamasha yanayofahamika kama Fashion Shows.

Nchini Kenya vijana wenye vipaji wanatumia matamasha hayo kutangaza bidhaa mbalimbali, kujipatia kipato na pia kuhamasisha jamii.

Maonyesho ya mitindo huwakutanisha vijana.
Maonyesho ya mitindo huwakutanisha vijana.

Angela Mumbi msichana mwenye umri wa miaka 24 mkaazi wa Mombasa, amekuwa mwanamitindo kwa miaka 4 sasa, na anaeleza kwanini aliamua kuingilia fani hii kama kijana.

Anasema anafanya uanamitindo kwa sababu kwake yeye ni talanta, halafu pia inampa furaha kama mwanamke anapokuwa jukwaani huwa anafurahi sana.

Kulingana na vijana hawa ni kuwa maonyesho ya urembo ni kazi wanayoitegemea, ambapo hutumia vipaji vyao kutangaza bidhaa na hata kupata kandarasi kutoka kwa kampuni mbalimbali.

Na licha ya kuwa chimbuko la uanamitindo ni katika mataifa ya Ulaya kama vile Ufaransa na Marekani, vijana wa kiafrika wanatumia fani hii kuonyesha utamaduni wa kiafrika kupitia mavazi kama wanavyoeleza.

Watayarishaji wa maonyesho ya bidhaa za urembo nchini Kenya maarufu kama Fashion Shows wanatumia fursa hiyo sio tu kuwapa ajira vijana wenye vipaji, lakini pia kuhamasisha kuhusu maadili mema katika jamii .

Erick Pamba ni mmoja wa watayarishaji wa matamasha ya urembo mjini Mombasa.

"Lengo letu la kuanzisha matamsha ni kutokana na jinsi jamii inachukulia kuwa Fashion inahusu ushoga kwa wanaume, na ukahaba kwa wasichana. Tunataka kuondoa hiyo dhana katika jamii na pia kuwasaidia vijana kujipatia kipato zaidi," anaeleza Pamba.

Hata hivyo Angela Mumbi anasema Afrika bado haijakumbatia vilivyo taaluma hii, na wazazi wengi wamekuwa wakiihusisha na ukahaba, hatua anayosema imekuwa changamoto kwao.

Kulingana naye ni kuwa wazazi wengi huzingatia kazi kama vile udaktari na uwakili, na kuwavunja moyo watoto wenye nia ya kuwa wanamitindo.

Lengo la vijana hawa ni kuonyesha mfano kwa vijana wengine Afrika mashariki na bara hili kwa ujumla, kuhusu kile wanaweza kufanya katika jamii, na pia kujipatia kipato kutokana na vipaji vyao.

XS
SM
MD
LG