Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umetangazwa nchini Uganda baada ya maafisa wa afya kuthibitisha kwamba mtu mmoja ameambukizwa na aina nadra ya virusi hiyo kutoka Sudan, wizara ya afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) zilisema Jumanne.
Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 24 katika wilaya ya kati ya Mubende nchini Uganda alionyesha dalili za ugonjwa huo na baadaye kufariki.
Tunataka kufahamisha nchi kuwa tuna mlipuko wa Ebola ambao tulithibitisha jana," Diana Atwine, katibu mkuu wa wizara ya afya, aliambia mkutano wa wanahabari.
Alisema mgonjwa aliyethibitishwa alikuwa na homa kali, kuharisha na maumivu ya tumbo na alikuwa akitapika damu. Awali alikuwa ametibiwa malaria.
Kwa sasa kuna watu wanane wanaohofiwa wameambukizwa na wamepewa huduma katika kituo cha afya, ofisi ya WHO barani Afrika ilisema katika taarifa yake, na kuongeza kuwa inasaidia maafisa wa afya wa Uganda katika uchunguzi wao na kupeleka wafanyakazi katika eneo lililoathiriwa.