Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 15, 2024 Local time: 02:56

Mkuu wa jeshi Somalia anusurika kifo


Kundi la wanamgambo wa al-Shabab ambalo linapambana na serikali ya Somalia
Kundi la wanamgambo wa al-Shabab ambalo linapambana na serikali ya Somalia
Mkuu wa jeshi nchini Somalia amenusurika shambulizi moja la bomu katika mji mkuu Mogadishu. Maafisa wa usalama nchini humo wanasema bomu lililotegwa kando ya bara bara lililipuka Jumatano wakati msafara wa gari maalumu lililombeba Jenerali Dahir Adan Elmi ukipita.

Kamanda wa jeshi aliiambia Idhaa ya Kisomali ya Sauti ya Amerika-VOA kwamba Jenerali Elmi yupo salama na kwamba hakuna mlinzi wake yeyote aliyejeruhiwa katika shambulizi hilo ambalo lilitokea katika wilaya ya Hodan wakati msafara huo ukielekea wizara ya ulinzi.

Polisi walifanya operesheni ya usalama baada ya mlipuko na waliwakamata watu takribani 30. Hakuna madai ya haraka ya uwajibikaji juu ya shambulizi hilo.

Jumamosi wapiganaji kutoka kundi la wanamgambo wa al-Shabab walishambulia jengo la bunge mjini Mogadishu. Shambulizi la bomu na bunduki lilisababisha vifo vya watu 18 wakiwemo baadhi ya washambuliaji.

Kundi hilo lenye uhusiano na al-Qaida linadai kuwajibika kwa shambulizi la bomu katika nchi jirani ya Djibouti ambalo liliuwa watu wasiopungua wawili. Shambulizi la Jumamosi lilitokea kwenye hoteli moja inayotumiwa na wageni kutoka nje.

Katika ujumbe kwa njia ya sauti msemaji wa kundi la al-Shabab alisema walikuwa wanawalenga wafanyakazi wa NATO.

Alisema shambulizi hilo lilikuwa ni kulipiza kisasi kwa Ufaransa kuingilia kati masuala ya kisiasa huko Jamhuri ya Afrika ya kati na kwa wanajeshi wa Djibouti kuisaidia serikali nchini Somalia.

Djibouti ambayo ni koloni la zamani la Ufaransa ina vituo vya kijeshi vya Ufaransa na Marekani. Imechangia wanajeshi wake katika jeshi la Umoja wa Afrika linalopambana na kundi la al-Shabab nchini Somalia.
XS
SM
MD
LG