Mkosoaji wa serikali ya Rwanda anayetumia ukurasa wake wa You Tube, kuikosoa serikali Dieudonne Niyonsenga, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela, na mahakama moja mjini Kigali.
Niyonsenga, ndiye mkosoaji wa hivi karibuni wa serikali mwenye wafuasi wengi kwenye You-tube, kuhukumiwa kufungwa katika taifa hilo la Afrika mashariki linalodhibiti vikali kimtandao, linalotawaliwa na kiongozi mmoja kwa miongo mitatu.
Wakili wake Gatera Gashabana amesema kwamba watakata rufaa mara moja ya hukumu hii dhidi ya Niyonsenga na hukumu hiyo sio haki. Niyonsenga ambaye kituo chake cha You-Tube cha Ishema TV, kina zaidi ya wafuasi milioni 15, alipatikana na hatia jana Alhamisi kwa mashtaka manne yakiwemo ya kugushi, kujifanya na kuwadhalilisha, maafisa wa serikali bila ya yeye kuwepo mahakamani.
Mahakama inaona kuwa makosa ambayo Niyonsenga, anahukumiwa nayo yalifanywa kwa makusudi, jaji alisema katika kutoa uamuzi huo ikiwa ni pamoja na faini ya faranga za Rwanda milioni tano, sawa na dola 4,900.
Kutokana na matokeo mabaya ambayo uhalifu wake umewasababishia jamii ya Rwanda, mahakama inaamuru Dieudonne Niyonsenga, akamatwe mara moja na apelekwe kutumikia kifungo chake jela.