Mkutano wa siku tatu wa kujadili mikakati ya utekelezaji wa mpango wa umoja wa mataifa wa kupambana na LRA umemalizika hii leo mjini Kampala. Mkutano huu ambao ulihudhuriwa na wajumbe kutoka DRC, Jamhuri ya Afrika ya kati, Uganda na Sudan kusini nchi ambazo zimeathiriwa na vitendo vya Joseph Kony uliafikiana kuwa kikosi cha pamoja cha kumsaka Kony kitaanza kazi hivi karibuni.
Hii sio mara ya kwanza kusikia matamshi kuwa Congo, Uganda, Sudan kusini na jamhuri ya afrika ya kati zineunda jeshi la pamoja ili kumsaka kiongozi wa LRA Joseph Kony na kundi lake. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi wa tatu mwaka huu wakati mjumbe maalum wa umoja wa afrika anayehusiana na masuala ya LRA balozi Franscisco Madeira alipowahakikishia waandishi habari kuwa kikosi hiki kingeundwa na kuanza kazi mara moja.
Kufikia leo, kikosi hiki hakijaanza kazi. Mikakati iliundwa vizuri na viongozi kuchaguliwa na hata kuapishwa lakini wanajeshi elfu tano waliotarajiwa kuunda jeshi hili hawamo. Hata hivyo balozi Madeira sasa anasema baada ya mkutano wao, majeshi yako njiani kwenda kambini.
Mashirika yasiyo ya serikali yanayofanya kazi kwenye maeneo ambayo yameathiriwa na vitendo vya LRA mkiwemo invisible children, enough, global centre for the responsibility to protect na resolve yanasema juhudi za kumsata Kony huenda zikachukua muda mrefu sana kwa sababu ya hali ya kutoaminiana kati ya serikali za nchi husika.
Wakati kikosi hiki kitakapoanza kazi, miongoni mwa maswala watakayotilia maanani ni kuwalinda wananchi wasivaamiwe na LRA, kuwasaidia waathiriwa kwa kuwapa makaazi, kuzisaidia serikali husika kudumisha usalama na kuhakikisha kuwa wanajeshi wana vifaa wanavyohitaji kupigana.
Huku baadhi ya waasi wa LRA wakiripotiwa kuwa Sudan kwenye eneo la Darfur, Sudan haitarajiwi kutoa majeshi yatakayounda kikosi hiki maalum lakini itashirikishwa kupitia njia za kidiplomasia, lengo likiwa kuishinikiza imkate Kony ingiwa ataingia nchini humo.