Mapigano mapya yamelipuka mjini Abdijan leo Jumatano huku majeshi ya rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara yakishambulia wapiganaji wanaomtii kiongozi aliyeondolewa madarakani Laurent Gbagbo.
Mashahidi wanasema milipuko na milio ya bunduki kubwa kubwa ilisikika katika eneo la Yopougon, nje kidogo ya Abdijan, na kusababisha wakazi wengi kukimbia kutafuta usalama kwingineko.
Serikali mpya ya Ouattara inajaribu kurejesha hali ya ushwari baada ya miezi minne ya ghasia za kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Maafisa wametoa wito wa utulivu lakini makundi ya wanamgambo yanaendelea kumwunga mkono Gbagbo ambaye alitiwa nguvuni na majeshi ya Ouattara wiki iliyopita, baada ya majeshi ya Ufaransa na Umoja wa Mataifa kushambulia makazi yake.