Katika ujumbe kwenye ukurasi wa Facebook wa Ikulu kiongozi huyo anasema kulitokea hali ya kutatanisha baada ya kundi la wanajeshi kufanya uasi ndani ya kambi kuu.
Damiba anasema mazungumzo yanaendelea kurudisha hali ya utulivu.
Hata hivyo wanajeshi wanaonekana wakishika zamu kando ya njia inayoelekea kwenye nyumba ya rais na kuzuia watu kuingia kwenye majengo ya serikali na kituo cha televisheni ya taifa, ambayo ilikuwa imesitisha matangazo kulingana na shirika la habari la Reuters.
Haijabainika bado kama hili lilikuwa jaribio la mapinduzi lakini lilikuwa na ishara zote za unyakuzi mwingine wa mamlaka ambao umekumba nchi za Afrika Magharibi na Kati katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Kikosi cha kijeshi kinachoongozwa na Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba kilichukua mamlaka Burkina Faso kutokana na mapinduzi ya Januari 24.
Mapinduzi hayo yalisherehekewa kwa kiasi kikubwa na raia waliochoshwa na serikali ya kiraia ya Rais wa zamani Roch Kabore ambayo haikuweza kuwadhibiti wapiganaji wa Kiislamu ambao wameua maelfu ya raia katika miaka ya hivi karibuni na kuteka maeneo makubwa ya kaskazini na mashariki.
Katika taarifa yake ya kwanza baada ya mapinduzi ya Januari, Damiba, ambaye mara nyingi huonekana hadharani katika sare za kijeshi na miwani ya jua aliahidi kurejesha usalama.
Lakini mashambulizi katika nchi hiyo maskini ya Afrika Magharibi yamezidi kuwa mbaya na jeshi liko katika hali mbaya. Watu wa kawaida ambao walimpa Damiba uungwaji mkono mwezi Januari, wamekasirishwa na ukosefu wa maendeleo, vyanzo vya usalama vinasema.