Hasira iliongezeka kutokana na hatua kali za China katika kukabiliana na janga la covid na kupelekea watu kumiminika mitaani mwishoni mwa Jumaa lililopita katika maandamano makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.
Kufuatia machafuko yaliyotokea kote China, mijii kadhaa imeanza kulegeza masharti ya kupambana na Covid, kama vile kuondoa masharti ya kulazimisha upimaji wa watu wengi kila siku, ambao ulikuwa msingi wa maisha ya kila siku chini ya sera kali ya Beijing ya kutopatikana hata kisa kimoja cha maambukizi ya Covid.
Kuanzia leo, mji mkubwa wa kusini magharibi wa Chengdu hautalazimisha tena watu kuonyesha kwamba walipimwa na hawakukutwa na maambukizi ili waruhusiwe kuingia kwenye maeneo ya umma au kusafiri na treni ya mwendo kasi, maarufu metro.