Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Mei 07, 2024 Local time: 22:54

Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Samia awataka vijana kuuenzi na kuulinda


Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wakati Tanzania ikiadhimisha siku ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, uliotimiza miaka 60 Ijumaa, Rais Samia Suluhu Hassan amewataka vijana nchini humo kuuenzi na kuulinda muungano.

Wakati huo huo vijana katika maadhimisho hayo wameitaka serikali kuwapatia elimu juu ya Muungano ili kuwasaidia kuufahamu kwa undani pamoja na kutatua changamoto zilizopo.

Sherehe za Muungano zimefanyika Jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Uhuru na kuhudhuriwa na Marais kutoka nchi 7 za Afrika ikiwemo Kenya, Burundi, Zambia, Somalia, Comoro na Namibia. Pia imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Kiserikali kutoka Barani Afrika.

Wakati akilihutubia taifa Rais Samia amewahimiza vijana kuulinda na kuuenzi Muungano kwa kuwa ni urithi na tunu ya Taifa la Tanzania na ni tunu ya Afrika kwa ujumla.

“Matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 yanatuonyesha kwamba idadi kubwa ya Watanzania ni vijana kwa kuzingatia hilo uimara na uendelevu upo mikononi mwa vijana. Nina wasihi sana vijana wote wa Tanzania muwe walinzi wa Muungano huu,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo bado vijana wamekuwa wakilalamika ukosefu wa elimu ya Muungano ambayo ilipaswa kutolewa ili kuwasaidia kufahamu haki zao na pia kufahamu mipaka yao katika muungano huo.

Kama anavyoeleza Adili Mansuri kutoka Amani Zanzibar: “Natoa wito kwa Serikali yangu ya Tanzania kupitia huu Muungano itupe elimu sana hasa sisi vijana, ili tujue ukomo wetu na mambo gani ni haki yako kuyapata katika huu Muungano na mambo ambayo labda sio haki yako kuyapata”.

Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wakiwa katika kilele cha sherehe za miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wakiwa katika kilele cha sherehe za miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kauli hiyo ya kutolewa kwa elimu inakuja baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za kikodi ambapo kwa Zanzibar wafanyabiashara hulazimika kulipa kodi mara mbili kwa ajili ya mizigo yao ya kibiashara.

Kama anavyoeleza Iddi Mwalimu kutoka Wete Pemba: “Vijana tunalalamikia haya maswala ya kodi hasa upande wa Zanzibar kwanini kwa upande wetu wanakata kodi mara mbili ZRA wanakata na TRA wanakata kodi pia na wakati Tanganyika kule hakuna ZRA iko TRA peke yake, hili linatuumiza sana vijana."

Adili Mansuri amesema kuwa vijana wa Zanzibar wamekuwa wakikutana na changamoto ya leseni za udereva kutotumika Tanzania bara suala ambalo linamlazimu kijana wa Zanzibar kukata leseni mpya anapokuja Tanzania bara.

“Unakuta mfano mimi ni dereva nimepata kazi Tanzania bara ninapofika kule leseni yangu ya udereva naambiwa kuwa hii haiwezi kufanya kazi huku kwasababu hiyo, leseni ya udereva Zanzibar kwa Tanzania bara haiwezi ikafanya kazi” ameongezea Adili.

Mohammed Mwaruhunga kutoka Tanga ameitaka serikali kuendelea kutatua changamoto za muungano ili kuhakikisha unakuwa ni muungano wenye tija na utakaoleta manufaa kwa pande zote mbili hasa vijana ambao wanatamani kufanya biashara Tanzania Bara na Visiwani.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika.

Forum

XS
SM
MD
LG