Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 02, 2022 Local time: 08:50

Mgonjwa wa kwanza athibitishwa kuwa na virusi vya corona Tanzania


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, Ummy Mwalimu

Mgonjwa wa kwanza mwenye homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ameripotiwa nchini Tanzania Jumatatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema mgonjwa huyo ambaye ni Mtanzania mwenye umri wa miaka 46 amegundulika kuwa na virusi hivyo baada ya kuwasili nchini katika uwanja wa Ndege wa kimataifa KIA akitokea Ubelgiji.

Waziri Ummy amesema mgonjwa huyo ambaye aliondoka nchini Machi 3 mwaka huu alitembelea nchi za Sweden na Denmark, ambapo akiwa Ubelgiji mume wa mwenyeji wake alikuwa mwathirika wa virusi vya Corona.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy mgonjwa huyo alitua uwanjani hapo na kufanyiwa ukaguzi na kuonekana hana homa, lakini baadae mgonjwa huyo alianza kujisikia vibaya akiwa hotelini na kwenda hospitali ya Mkoa ya Mt. Meru.

Hatua zilizofuatia ni sampuli ilichukuliwa na kupelekwa maabara ya taifa ya afya ya jamii iliyopo Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi na kubainika mgonjwa huyo ana virusi vya Corona.

Hata hivyo Waziri Ummy amewatoa hofu Watanzania kwamba serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ili usiweze kusambaa nchini.

Ummy amesema, Waziri Mkuu, mh Kassim Majaliwa muda wowote kuanzia sasa anatarajiwa kukutana na mawaziri 12 wa sekta mbalimbali ili kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huo ambao umesambaa katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya duniani (WHO) hapa nchini, Dk Tigest Katsela Mengestu, amesema ugonjwa wa Corona umekuwa tishio katika nchi mbalimbali, huku akiipongeza serikali ya Tanzania kutokana na hatua inazozichukua katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG