Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Aprili 27, 2025 Local time: 06:35

Mgomo wa wafanyabiashara Uganda Unaendelea.


Mgomo wa wafanya biashara wa Uganda umesababisha magari ya abiria kutokua na biashara nzuri.
Mgomo wa wafanya biashara wa Uganda umesababisha magari ya abiria kutokua na biashara nzuri.

Wafanyabiashara wasema serikali na benki kuu hazina utashi wa kuwapunguzia kiwango cha riba na kuapa kuendelea na mgomo wao.

Mgomo wa siku tatu wa wafanyabiashara mjini kampala unaendelea baada ya mkutano kati ya rais Yoweri Museveni na wanachama wa shirika la wafanyabiashara - KACITA kugonga mwamba hapo jana.

Rais Museveni aliwaambia wafanyabiashara wayafungue maduka akisema kugoma sio suluhu na kupendekeza majadiliano kama njia muafaka ya kuona ni vipi wanaweza kupunguza kiwango kikubwa cha riba wanacholipa.

Wafanyabiashara wachache walifungua maduka yao jambo ambalo liliwakera wafanyabiashara wenzao waliokuwa wamefunga maduka yao mjini Kampala.

Waliokuwa wamefunga maduka waliwakaripia wenzao na kuwalazimisha kufunga maduka yao pia. Wafanyabiashara wanasema serikali na benki kuu hazina utashi wa kuwapunguzia kiwango cha riba wanacholipa na kuapa kuendelea na mgomo wao.

Hata hivyo, benki kuu imewalaumu wafanya biashara kwa kuchukua mikopo na kutia saini mikataba ambayo hawaielewi. Msemaji wa benki kuu nchini Uganda Jan Tibamwenda alisema benki kuu haifai kulaumiwa hata kidogo kwa sababu wakati mtu anapochukua mkopo kutoka benki, anapewa fursa ya kuchagua kama anataka kutozwa kiasi kisichobadilika cha riba ama anataka kutozwa riba ambayo inabadilika kulingana na mfumuko wa bei.

Wengi wa wafanyabiashara walitia saini mikopo ambayo kiwango chake cha riba kinabadilika kulingana na mfumuko wa bei.

Mgomo huu umewaathiri wafanyabiashara kutoka nchi nyingine ambao huenda Uganda kununua bidhaa za kuuza nchini mwao.

Na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara - KACITA walikuwa wanakutana na wafanyabiashara kuona ni mwelekeo upi watakaouchukua.

Rais Yoweri Museveni anatarajiwa kukutana wa wafanyabiashara hapo kesho ili kutatua mzozo huu ambao anasema unaweza kuwatisha wawekezaji ambao wangependa kuwekeza nchini Uganda.

XS
SM
MD
LG