Madaktari nchini Tanzania wamesema hawawezi kukubali kufungwa midomo ili kuacha kutetea maslahi yao na wananchi kwa ujumla.
Ktika kongamano la madaktari lililofanyika Ijumaa na kuhusisha zaidi ya madaktari 400, wengi wamehoji na kutoa misimamo yao kuhusu kupigwa na kutupwa kinyama kwa katibu wa jumuiya ya madktari nchini humo Dk. Stephen Ulmboka, kufutiwa leseni kwa muda kwa madaktari 400 walioko mafunzoni (interns) na kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari nchini humo Dk. Namala Nkopi na kuwekwa mazingira bora katika hospitali za Serikali .
Akizungumza baada ya mkutano huo katibu wa jumuiya ya madaktari nchini Tanzania Dk.Edwin Chitage amesema maazimio yaliyotolewa baada ya mkutano ni kuendelea kuishinikiza serikali kutatua madai yao ili waweze kufanya kazi kwa amani. Amesema kamwe hawata sita kusema ukweli wala kudai haki zao kwa kuiogopa serikali.
Hoja ya Dk.Ulimboka bado ni kitendawili katika mzozo huu kwa vile tangu kuundwa kwa tume ya uchunguzi inayotarajiwa kutoa ripoti ya kupigwa, kunyanyaswa na kisha kutupwa kwa daktari huyu, hadi sasa imedaiwa kwamba hakuna tamko lolote lililotolewa au kuelezwa jinsi uchunguzi unavyoendelea.
Wakati hayo yakitokea bado wananchi wa Tanzania wanaendelea kutaabika, kutokuwa na imani na hospitali za Serikali na wengine kukimbilia zaidi katika hospitali binafsi.
Madaktari wanatarajia kufanya maandamano makubwa jijini Dar es salaam kupinga kile walichokiita unyanyasaji dhidi yao wakati wanapodai haki zao na wananchi kwa ujumla.