Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 09, 2022 Local time: 09:53

Mgomo wa madaktari wasababisha vifo Kenya


Mgomo wa madaktari nchini Kenya

Athari ya mgomo wa madaktari, hasa ukizingatia namna ambavyo wagonjwa wanahangaika, ni kielelezo cha kutosha juu ya hatari zinazowakabili wananchi wa hali ya chini nchini Kenya.

Michael Sunday ni mkazi wa chokaa mtaa wa Ruai hapa jijini Nairobi, amempoteza mkewe Doreen Kitonga katika siku kumi wakati mgomo unaendelea na pengine kuna wengi ambao tayari wamesha poteza maisha.

Kwa mujibu wa Michael mkewe aliyepata majeraha baada ya kuunguwa na moto wakati akiwa anapika alikimbizwa Hospitali. Mgomo huu tayari umeingia mwezi wa tatu.

Michael ameelezea masikitiko yake makubwa kwamba: “Wakati mke wangu alipopata ajali hiyo tulimkimbiza Hospitali ya St Francis na tukaambiwa tumpeleke hospitali ya Kenyatta kwa sababu kulikuwa hakuna madaktari.

Anasimulia alilazwa siku mbili tatu na akaanza kupata nafuu lakini baadae aliaga dunia.

Jambo ambalo linamtatiza Michael ni kukosa kufahamu kilicho sababisha kifo cha mkewe.

Wataalamu wa Afya

Lakini wataalamu wa afya wanasema kuwa ajali ya moto daraja la tatu ni hatari na inahitaji matibabu ya papo kwa papo. Mtu anatakiwa apelekwe hospitali mara moja na kupata matibabu.

Ajali kama hii huwa inaathiri tabaka zote za ngozi na mafuta yaliyoko chini yake kwamba mkewe michael inawezekana alichelewa kupata matibabu.

Mjini Mombasa sawa na miji mingine wagonjwa wamelazimika kutafuta matibabu katika hospitali za kibinafsi, japo gharama ya matibabu ni kubwa katika hospitali hizo.

Billy Ochieng ambaye mtoto wake wa umri wa miezi nane amelazwa hospitali ya Mombasa kufanyiwa upasuaji anasema mgomo wa madaktari umekuwa changamoto kubwa kwake. Sasa amelazimika kwenda hospitali ya binafsi ya Mombasa kupata huduma.

Billy Ochieng anaelezea namna mgomo huu ulivyo muathiri akisema: “Mimi mara ya kwanza nimetumia laki moja………tusingeweza kumuacha mtoto aendelee hivi.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa madaktari wameendelea kushikilia kuwa lazima mkataba wa makubaliano wa 2013 uliofikiwa kati yao na serikali utekelezwe.

Shinikizo la Serikali

Anasema kuwa Serikali kuu pamoja na serikali za kaunti zimeendelea kusisitiza kutokuwapo kwa mkataba wa makubaliano unaodaiwa na madaktari.

Serikali inashikilia kuwa mkataba huo haukupata baraka za Tume ya kurekebisha mishahara ya wafanyakazi wa Umma na kutaka makubaliano mengine yafanyike chini ya Tume hiyo, jambo ambalo linaonekana kuwakasirisha madaktari.

Mahakama ya kushughulikia maslahi ya wafanyakazi mwishoni mwa wiki imeamrisha pande husika kuafikiana kupata suluhu chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi nchini Francis Atwoli, kabla ya tarehe kumi na tatu mwezi huu na kuikabidhi mahakama hiyo ripoti kamili.

Katika hospitali ya umma ya Mbagathi hapa jijini Nairobi, maeneo mengi ya kupokea wagonjwa ni matupu, vitanda vinaonekana havijalaliwa.

Daktari Tuimising Loice anasema wadi zote hazina wagonjwa na hakuna kazi inayoendelea. Lakini upande wa wagonjwa wanaotibiwa na kurudi nyumbani, ni kati ya mia mbili hadi mia tatu. Kati yao ni watoto wanaoletwa kwa ajili ya kupatiwa chanjo.

“Hawa ni kundi la watu ambao wanahudumiwa kila siku na wahudumu wa afya, japokuwa kabla ya mgomo wagonjwa walikuwa kati ya 700-900.”

Daktari Benard Muia Afisa Mkuu wa Wizara ya matibabu katika Kaunti ya Nairobi anaeleza kuwa inasikitisha mno kuwaona madaktari barabarani huku wagonjwa wakiendelea kutaabika.

Ameeleza kuwa: “Kusema kweli idadi ya wagonjwa imepungua kufuatia mgomo, tulikuwa tunalaza wagonjwa wengi hapa sasa idadi ya wanaolazwa imeshuka hadi kufikia asilimia 10.”

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG