Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:24

Mgogoro wa almasi Zimbabwe waendelea.


Nchini Zimbabwe mshitakiwa Farai Maguwu amenyimwa dhamana tena jana, pale mahakama kuu ya Harare iliposema kuwa mashtaka yanayomkabili ni makubwa.

Hakimu wa mahakama kuu Zimbabwe Chinembiri Bhunu alisema jana mahakamani kuwa alikubaliana na hukumu ya wiki ilopita kutoka mahakama ndogo kuwa Farai Maguwu anakabiliwa na mashtaka magumu na kwamba polisi lazima wapewe muda zaidi kuchunguza tuhuma za uhalifu alofanya.

Afisi ya mwana sheria mkuu inamshutumu Maguwu kwa kuchapisha habari za uwongo zinazodhuru nchi yake.

Maguwu alikamatwa Juni 3, na anakana mashtaka ya kuwa na maelezo ya uwongo juu ya mauwaji, mateso, na majina ya wahusika pamoja na nyaraka za serikali ziloibwa, yote yakiwa mashtaka yanayoweza kupewa hukumu ya hadi miaka 20 jela.

Maguwu alikamatwa siku tu baada ya kukutana na mfuatiliaji maalum wa almasi kutoka Afrika kusini wa Kimberely Process, kwa Zimbabwe Abbey Chikane.

Chikane aliripoti kwa serikali kuwa Maguwu alimpatia nyaraka za siri za serikali ya Zimbabwe zinazoshutumiwa kuwa zinahusu shughuli za kijeshi katika machimbo hayo ya almasi yenye ubishi, katika eneo la Marange huko kusini-mashariki mwa Zimbabwe.

Wakili wa Maguwu, Tino Bere, alisema jana kuwa mteja wake hana afya nzuri. Anasema hajapatiwa mablanketi huko jela ambako kuna baridi nyingi, na kwamba sasa amepata madhara mabaya ya kifua na koo.

Mahakama ilimkubalia Maguwu kulazwa katika hospitali ya kibinafsi mjini Harare, ambapo alifanyiwa operesheni kwenye koo lake.

Bere anasema daktari wa jela alimtembelea Maguwu hospitalini jana, na kwamba mteja wake sasa atahamishwa hadi kwenye hospitali ya jela ya Zimbabwe ili ahudumiwe zaidi baada ya operesheni.

Pale ombi la kuachiliwa kwa dhamana kwa Maguwu lilipokuwa linasikilizwa huko mahakamani mjini Harare, Kimberely Process ilikuwa inakutana huko Tel Aviv. Kipaumbele cha ajenda yake ni ripoti ya Chikane kuhusu Zimbabwe.

Kundi la Human Rights Watch pia lilikuwepo kwenye mkutano huko mjini Tel Aviv, nalo lilisema Zimbabwe inafaa kuzuiliwa kutoka Kimberly Process kwa sababu ya ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadam dhidi ya wachimba almasi wasio rasmi

Human Rights Watch inasema almasi zilochimbwa huko mashariki mwa Zimbabwe zinafaa kutambulishwa kuwa ni almasi za damu.

Mkutano huo huko Tel Aviv unamalizika hapo kesho.

XS
SM
MD
LG